Yohana - Sura ya 9

1Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa.
2Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?
3Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.
4Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi.
5Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.
6Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,
7akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona.
8Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba?
9Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye.
10Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje?
11Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona.
12Wakamwambia, Yuko wapi huyo? Akasema, Mimi sijui.
13Basi wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani.
14Nayo ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho.
15Basi Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona. Akawaambia, Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona.
16Basi baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato. Wengine wakasema, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo? Kukawa matengano kati yao.
17Basi wakamwambia yule kipofu mara ya pili, Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho? Akasema, Ni nabii.
18Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona.
19Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa?
20Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu;
21lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.
22Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi.
23Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye.
24Basi mara ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu, wakamwambia, Mpe Mungu utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi.
25Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona.
26Basi wakamwambia, Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani?
27Akawajibu, Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?
28Basi wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake yule; sisi tu wanafunzi wa Musa.
29Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako.
30Yule mtu akajibu, akawaambia, Hii ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho!
31Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo.
32Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo.
33Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.
34Wakajibu, wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje.
35Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?
36Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?
37Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.
38Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia.
39Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.
40Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?
41Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.