Yona - Sura ya 2

1Ndipo Yona akamwomba Bwana, Mungu wake, katika tumbo la yule samaki,
2Akasema, Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu.
3Maana ulinitupa vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu.
4Nami nikasema, Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu.
5Maji yalinizunguka, hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu;
6Nalishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi na mapingo yake yalinifunga hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka shimoni, Ee Bwana, Mungu wangu,
7Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nalimkumbuka Bwana; Maombi yangu yakakuwasilia, Katika hekalu lako takatifu.
8Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo Hujitenga na rehema zao wenyewe;
9Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu. Wokovu hutoka kwa Bwana.
10Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.