Yoshua - Sura ya 13

Yoshua - Sura ya 13

1Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, Bwana akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa.

2Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote;

3kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; mashehe matano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi,

4upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori;

5na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa kuelekea maawio ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikilia maingilio ya Hamathi;

6na watu wote wenye kuikaa nchi ya vilima kutoka Lebanoni hata Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru.

7Basi sasa gawanya nchi hii, iwe urithi wa hizi kabila kenda, na nusu ya kabila ya Manase.

8Pamoja na yeye, Wareubeni na Wagadi walipata urithi wao, waliopewa na Musa, huko ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, vile vile kama huyo Musa mtumishi wa Bwana alivyowapa;

9kutoka huko Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Amoni, na huo mji ulio pale katikati ya bonde, na nchi tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni;

10na miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni, hata mpaka wa wana wa Amoni;

11na Gileadi na mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na mlima wa Hermoni wote, na Bashani yote mpaka Saleka;

12ufalme wote wa Ogu uliokuwa katika Bashani, huyo aliyekuwa akitawala katika Ashtarothi na katika Edrei (huyo alisalia katika mabaki ya wale Warefai); kwa kuwa Musa aliwapiga hao na kuwafukuza.

13Pamoja na hayo wana wa Israeli hawakuwafukuza Wageshuri, wala Wamaaka; lakini Wageshuri na Wamaaka wamekaa kati ya Israeli, hata siku hii ya leo.

14Lakini hakuwapa watu wa kabila ya Lawi urithi uwao wote; maana sadaka za Bwana, Mungu wa Israeli, zisongezwazo kwa njia ya moto ndizo urithi wake huyo, kama alivyomwambia.

15Musa akawapa kabila ya wana wa Reubeni kwa kadiri ya jamaa zao.

16Mpaka wao ulikuwa kutoka hapo Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Arnoni, na huo mji ulio katikati ya bonde, na nchi tambarare yote iliyo karibu na Medeba;

17na Heshboni na miji yake yote iliyoko katika bonde; na Diboni, na Bamoth-baali, na Beth-baal-meoni;

18na Yahasa, na Kedemothi, na Mefaathi;

19na Kiriathaimu, na Sibma, na Sereth-shahari katika kilima cha hilo bonde;

20na Beth-peori, na nchi za matelemko ya Pisga, na Beth-yeshimothi;

21na miji yote ya nchi tambarare, na ufalme wote wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akitawala katika Heshboni, aliyepigwa na Musa pamoja na hao wakubwa wa Midiani, nao ni Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao mashehe wa Sihoni, waliokuwa katika nchi hiyo.

22Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.

23Na mpaka wa wana wa Reubeni ulikuwa ni mto wa Yordani, na mpaka wake. Huo ndio urithi wa wana wa Reubeni sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake.

24Musa akawapa kabila ya Gadi, hao wana wa Gadi, kwa kadiri ya jamaa zao.

25Mpaka wao ulikuwa ni Yazeri, na miji hiyo ya Gileadi, na nusu ya nchi ya wana wa Amoni, mpaka Aroeri uliokabili Raba;

26tena kutoka Heshboni mpaka Ramath-Mizpe, na Betonimu; tena kutoka Mahanaimu hata mpaka wa Debiri;

27tena katika bonde, Beth-haramu, na Bethnimira, na Sukothi, na Safoni, hiyo iliyosalia ya ufalme wa Sihoni mfalme wa Heshboni, yaani mto wa Yordani na mpaka wake, mpaka mwisho wa bahari ya Kinerethi ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki.

28Huo ndio urithi wa wana wa Gadi sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake.

29Kisha Musa akawapa hao wa nusu ya kabila ya Manase urithi wao; ulikuwa ni wa hiyo nusu ya kabila ya wana wa Manase sawasawa na jamaa zao.

30Na mpaka wao ulikuwa kutoka huko Mahanaimu, Bashani yote, na ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, na miji yote ya Yairi, iliyo katika Bashani, miji sitini;

31na nusu ya Gileadi, na Ashtarothi, na Edrei, hiyo miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani, ilikuwa ni ya wana wa Makiri mwana wa Manase maana, kwa hiyo nusu ya wana wa Makiri sawasawa na jamaa zao.

32Hizi ndizo mirathi ambazo Musa alizigawanya katika nchi tambarare za Moabu, ng'ambo ya pili ya Yordani, kukabili Yeriko, upande wa mashariki.

33Lakini Musa hakuwapa kabila ya Lawi urithi uwao wote; yeye Bwana, Mungu wa Israeli, ndiye urithi wao, kama alivyowaambia.