Yoshua - Sura ya 16

Yoshua - Sura ya 16

1Kura ya wana wa Yusufu ilianza kutoka mto wa Yordani hapo Yeriko, hapo penye maji ya Yeriko upande wa mashariki, maana, ni hiyo nyika, kukwea kutoka Yeriko kati ya hiyo nchi ya vilima mpaka Betheli;

2kisha ikatoka huko Betheli kwendelea Luzu, kisha ikaendelea hata kuufikilia mpaka wa Waarki mpaka Atarothi;

3kisha ikatelemkia upande wa magharibi hata kuufikilia mpaka wa Wayafleti, hata mpaka wa Beth-horoni ya chini, hata kufikilia Gezeri; na matokeo yake yalikuwa hapo baharini.

4Na wana wa Yusufu, Manase na Efraimu, walitwaa urithi wao.

5Na mpaka wa wana wa Efraimu kwa kuandama jamaa zao ulikuwa hivi; mpaka na urithi wao upande wa mashariki ulikuwa ni Ataroth-adari, hata Beth-horoni wa juu;

6kisha mpaka ukatokea kwendelea upande wa magharibi huko Mikmeta upande wa kaskazini; kisha mpaka ukazunguka kwendea upande wa mashariki hata Taanath-shilo, kisha ukaendelea upande wa mashariki wa Yanoa;

7kisha ulitelemka kutoka Yanoa hata Atarothi, na Naara, kisha ukafikilia Yeriko, na kutokea hapo penye mto wa Yordani.

8Kutoka hapo Tapua mpaka ukaendelea upande wa magharibi hata kijito cha Kana; na matokeo yake yalikuwa baharini. Huo ndio urithi wa hao wana wa Efraimu kwa kuandama jamaa zao;

9pamoja na ile miji iliyotengwa kwa ajili ya wana wa Efraimu katikati ya urithi wa hao wana wa Manase, miji yote pamoja na vijiji vyake.

10Nao hawakuwatoa Wakanaani waliokuwa Wakikaa Gezeri; lakini hao Wakanaani waliketi kati ya Efraimu, hata hivi leo, wakawa watumishi wa kufanya kazi za shokoa.