Yoshua - Sura ya 21

Yoshua - Sura ya 21

1Wakati huo hao vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi wakamwendea Eleazari, kuhani, na Yoshua, mwana wa Nuni, na hao waliokuwa vichwa vya nyumba za mababa ya kabila za wana wa Israeli;

2wakanena nao hapo Shilo katika nchi ya Kanaani, wakisema, Yeye Bwana aliamuru kwa mkono wa Musa kwamba sisi tupewe miji tupate kukaa humo, pamoja na malisho yake kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo.

3Basi wana wa Israeli wakawapa Walawi miji hii, pamoja na malisho yake, katika urithi wao, sawasawa na hiyo amri ya Bwana.

4Kura ikatokea kwa ajili ya jamaa za Wakohathi; na wana wa Haruni kuhani, waliokuwa katika Walawi, walipata miji kumi na mitatu kwa kura katika kabila ya Yuda, na katika kabila ya Simeoni, na katika kabila ya Benyamini.

5Kisha Wakohathi wengine waliosalia walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Efraimu, na katika kabila ya Dani, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, miji kumi.

6Tena wana wa Gershoni walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Isakari, na katika kabila ya Asheri, na katika kabila ya Naftali, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase huko Bashani, miji kumi na mitatu.

7Na wana wa Merari kwa kuandama jamaa zao walipata katika kabila ya Reubeni, na katika kabila ya Gadi, na katika kabila ya Zabuloni, miji kumi na miwili.

8Kisha wana wa Israeli waliwapa Walawi kwa kura miji hiyo pamoja na malisho yake, kama Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa.

9Kisha wakawapa katika kabila ya wana wa Yuda, na katika kabila ya wana wa Simeoni, miji hii iliyotajwa hapa kwa majina;

10nayo ilikuwa kwa ajili ya wana wa Haruni, wa jamaa ya Wakohathi, waliokuwa wa wana wa Lawi; kwa kuwa kura ya kwanza ilikuwa ni yao.

11Nao wakawapa Kiriath-arba, huyo Arba alikuwa baba yake Anaki, (ndio Hebroni), katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na malisho yake yaliyouzunguka pande zote.

12Lakini mashamba ya mji, na vile vijiji vyake, wakampa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake.

13Kisha wakawapa wana wa Haruni kuhani Hebroni pamoja na malisho yake, huo mji wa kukimbilia kwa ajili ya mwuaji, na Libna pamoja na malisho yake;

14na Yatiri pamoja na malisho yake, na Eshtemoa pamoja na malisho yake;

15na Holoni pamoja na malisho yake, na Debiri pamoja na malisho yake;

16na Aini pamoja na malisho yake, na Yuta pamoja na malisho yake, na Bethshemeshi pamoja na malisho yake; miji kenda katika kabila hizo mbili.

17Tena katika kabila ya Benyamini, Gibeoni pamoja na malisho yake, na Geba pamoja na malisho yake;

18na Anathothi pamoja na malisho yake, na Almoni pamoja na malisho yake; miji minne.

19Miji yote ya wana wa Haruni, makuhani, ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na malisho yake.

20Na jamaa za wana wa Kohathi, Walawi, hao wana wengine wa Kohathi waliosalia, wao walikuwa na miji ya kura yao katika kabila ya Efraimu.

21Nao wakawapa Shekemu pamoja na malisho yake, katika nchi ya vilima ya Efraimu, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji; na Gezeri pamoja na malisho yake;

22na Kibisaumu pamoja na malisho yake, na Beth-horoni pamoja na malisho yake, miji minne.

23Tena katika kabila ya Dani Elteke pamoja na malisho yake, na Gibethoni pamoja na malisho yake;

24na Aiyaloni pamoja na malisho yake, na Gath-rimoni pamoja na malisho yake; miji minne.

25Tena katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, Taanaki pamoja na malisho yake, na Gath-rimoni pamoja na malisho yake; miji miwili.

26Miji yote ya jamaa za wana wa Kohathi waliosalia ilikuwa ni miji kumi, pamoja na malisho yake.

27Tena wana wa Gershoni, katika jamaa za Walawi, waliwapa, katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, Golani katika Bashani pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji; na Beeshtera pamoja na malisho yake; miji miwili.

28Tena katika kabila ya Isakari, Kishioni pamoja na malisho yake, na Daberathi pamoja na malisho yake;

29na Yarmuthi pamoja na malisho yake, na Enganimu pamoja na malisho yake; miji minne.

30Tena katika kabila ya Asheri, Mishali pamoja na malisho yake, na Abdoni pamoja na malisho yake;

31na Helkathi pamoja na malisho yake, na Rehobu pamoja na malisho yake; miji minne.

32Tena katika kabila ya Naftali, Kedeshi katika Galilaya pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji, na Hamoth-dori pamoja na malisho yake, na Kartani pamoja na malisho yake; miji mitatu.

33Miji yote ya Wagershoni kwa kuandama jamaa zao ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na malisho yake.

34Tena jamaa za wana wa Merari, hao Walawi waliosalia, katika kabila ya Zabuloni, Yokneamu pamoja na malisho yake, na Karta pamoja na malisho yake,

35na Dimna pamoja na malisho yake, na Nahalali pamoja na malisho yake; miji minne.

36Tena katika kabila ya Reubeni, Bezeri pamoja na malisho yake, na Yahasa pamoja na malisho yake,

37na Kedemothi pamoja na malisho yake, na Mefaathi pamoja na malisho yake; miji minne.

38Tena katika kabila ya Gadi Ramothi katika Gileadi pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji, na Mahanaimu pamoja na malisho yake;

39na Heshboni pamoja na malisho yake, na Yazeri pamoja na malisho yake; jumla yake miji minne.

40Miji hiyo yote ilikuwa ni miji ya wana wa Merari kwa kuandama jamaa zao, ni hizo jamaa za Walawi zilizosalia; na kura yao ilikuwa ni miji kumi na miwili.

41Miji yote ya Walawi iliyokuwa kati ya milki ya wana wa Israeli ilikuwa ni miji arobaini na minane, pamoja na malisho yake.

42Miji hiyo kila mmoja ulikuwa pamoja na malisho yake, yaliyouzunguka pande zote; ndivyo ilivyokuwa katika miji hiyo yote.

43Basi Bwana aliwapa Israeli nchi hiyo yote, ambayo aliapa kwamba atawapa baba zao; nao wakaimiliki, na kukaa mumo.

44Kisha Bwana akawapa raha pande zote, sawasawa na hayo yote aliyokuwa amewaapia baba zao; wala katika adui zao wote hakusimama hata mtu mmoja miongoni mwao mbele zao; yeye Bwana akawatia adui zao wote mikononi mwao.

45Halikuanguka neno lo lote katika jambo lo lote lililokuwa ni jema ambalo Bwana alikuwa amelinena katika habari ya nyumba ya Israeli; yalitimia mambo yote.