Yoshua - Sura ya 8

Yoshua - Sura ya 8

1Kisha Bwana akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake;

2nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma.

3Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu thelathini elfu, watu mashujaa wenye uwezo, akawapeleka wakati wa usiku.

4Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote;

5na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao;

6nao watatoka nje watufuate, hata tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao;

7basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu.

8Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la Bwana; angalieni, nimewaagiza.

9Basi Yoshua akawatuma; nao wakaenda hata hapo watakapootea, wakakaa kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa Ai; lakini Yoshua akalala usiku huo kati ya watu.

10Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakutanisha watu, kisha akatangulia kukwea kwenda Ai mbele ya hao watu, yeye na wazee wa Israeli.

11Watu wote, hao wa vita, waliokuwa pamoja naye, wakaenda wakakaribia, na kufikilia mbele ya mji, wakatua upande wa kaskazini wa Ai; napo palikuwa na bonde kati ya yeye na Ai.

12Kisha akatwaa watu kama elfu tano, akawaweka kuotea kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa huo mji.

13Basi wakawaweka hao watu, jeshi zima lililokuwa upande wa kaskazini wa mji, na wale waliokuwa waotea upande wa magharibi wa mji; naye Yoshua akaenda usiku huo katikati ya hilo bonde.

14Kisha ikawa hapo huyo mfalme wa Ai alipoona jambo hilo, ndipo walipofanya haraka, na wakaamka asubuhi na mapema, na watu waume wa mji wakatoka nje waende kupigana na Israeli, yeye na watu wake wote, kwa wakati ulioamriwa, kuikabili Araba; lakini hakujua ya kwamba walikuwako waviziao kinyume chake kwa upande wa nyuma wa mji.

15Kisha Yoshua na watu wa Israeli wote walifanya kana kwamba wameshindwa mbele yao, wakakimbia kwa njia ya nyika.

16Watu wote waliokuwa ndani ya mji waliitwa wakusanyike pamoja ili kuwafuatia; nao wakamfuatia Yoshua, wakasongea mbele na kuuacha mji.

17Hakusalia mtu ye yote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.

18Kisha Bwana akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji.

19Wale watu waliovizia wakainuka kwa upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji.

20Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kuenenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia.

21Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai.

22Tena hao; wengine wakatoka nje kuutoka huo mji kinyume chao; basi hivyo walikuwa wa katikati ya Israeli, wengine upande huu na wengine upande huu; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona.

23Kisha wakamshika mfalme wa Ai ali hai, nao wakamleta kwa Yoshua.

24Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga.

25Wote walioanguka siku hiyo waume kwa wake, walikuwa ni kumi na mbili elfu, yaani, watu wote wa mji wa Ai.

26Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hata hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai.

27Isipokuwa wanyama wa mji na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la Bwana alilomwamuru Yoshua.

28Basi Yoshua akaupiga moto mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni chungu ya magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo.

29Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hata wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake chungu kubwa ya mawe, hata hivi leo.

30Ndipo Yoshua alijenga madhabahu kwa Bwana, Mungu wa Israeli katika mlima Ebali.

31Kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyowaamuru wana wa Israeli, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo mtu hakutumia juu yake chombo cha chuma; nao wakatoa juu yake sadaka za kuteketezwa kwa Bwana, na kuchinja sadaka za amani.

32Akaandika huko juu ya mawe hayo nakala ya torati ya Musa, aliyoiandika mbele ya wana wa Israeli.

33Na Israeli wote, na wazee wao, na maakida yao, na makadhi yao, wakasimama upande huu wa sanduku na upande huu, mbele ya makuhani Walawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, huyo aliyekuwa mgeni pamoja na huyo mzalia; nusu yao mbele ya mlima Gerizimu, na nusu yao mbele ya mlima Ebali, kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyoamuru, ili wawabarikie watu wa Israeli kwanza.

34Na baadaye alisoma maneno yote ya torati, baraka na laana, sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati.

35Hapakuwa na hata neno moja katika hayo aliyoamuru Musa, ambalo Yoshua hakulisoma mbele ya kusanyiko lote la Israeli, na mbele ya wanawake, na watoto, na wageni waliokaa nao.