Waamuzi - Sura ya 1

Waamuzi - Sura ya 1

1Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza Bwana, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao?

2Bwana akasema, Yuda atakwea; tazama, nimeitia hiyo nchi mkononi mwake.

3Ndipo Yuda akamwambia Simeoni ndugu yake, Kwea wewe pamoja nami katika kura yangu, ili tupate kupigana na Wakanaani; kisha mimi nami nitakwenda pamoja nawe katika kura yako. Basi Simeoni akaenda pamoja naye.

4Yuda akakwea; naye Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mkononi mwao; nao wakawapiga huko Bezeki watu elfu kumi.

5Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi.

6Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya miguu.

7Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko.

8Kisha wana wa Yuda wakapigana na Yerusalemu, wakautwaa, wakaupiga kwa makali ya upanga, na kuupiga moto huo mji.

9Baadaye wana wa Yuda wakatelemka ili wapigane na hao Wakanaani waliokaa katika nchi ya milimani, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela.

10Kisha Yuda akawafuatia hao Wakanaani waliokaa katika Hebroni; (jina la Hebroni hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-arba;) nao wakamwua Sheshai, na Ahimani, na Talmai.

11Kisha kutoka hapo akawafuatia wale wenye kukaa Debiri. (Jina la Debiri hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-seferi.)

12Huyo Kalebu alisema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, nitamwoza mwanangu Aksa awe mkewe.

13Naye Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, aliutwaa; basi akamwoza mwanawe Aksa.

14Ikawa hapo alipokwenda kukaa naye, huyo mwanamke akamtaka ili aombe shamba kwa baba yake; na huyo mwanamke akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Una haja gani utakayo?

15Mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa wewe umeniweka katika nchi ya Negebu, basi unipe na vijito vya maji pia. Kalebu akampa vile vijito vya maji vya juu na vijito vya chini.

16Hao wana wa Mkeni, huyo shemeji yake Musa, wakakwea juu kutoka katika huo mji wa mitende, pamoja na wana wa Yuda, na kuingia hiyo nyika ya Yuda, iliyo upande wa kusini wa Aradi; nao wakaenda na kukaa pamoja na watu hao.

17Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na wakawapiga Wakanaani waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma.

18Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake.

19Bwana alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma.

20Kisha wakampa huyo Kalebu Hebroni, kama alivyonena Musa naye akawafukuza wale wana watatu wa Anaki.

21Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mji wa Yerusalemu; bali Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Benyamini ndani ya Yerusalemu hata hivi leo.

22Nyumba ya Yusufu nayo, wao nao walikwea kwenda juu ya Betheli; naye Bwana alikuwa pamoja nao.

23Kisha mbari ya Yusufu wakatuma watu waende kuupeleleza Betheli. (Jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Luzu.)

24Hao wapelelezi walimwona mtu atoka katika huo mji, wakamwambia, Tafadhali, utuonyeshe maingilio ya mji huu, nasi tutakutendea mema.

25Basi akawaonyesha maingilio ya mji, nao wakaupiga huo mji kwa makali ya upanga; lakini huyo mtu walimwacha aende zake, na watu wote wa jamaa yake.

26Huyo mtu akaenda katika nchi ya Wahiti, akajenga mji, akaliita jina la huo mji Luzu; nalo ndilo jina lake hata hivi leo.

27Tena Manase hakuwatoa wenyeji wa Bethsheani na miji yake, wala hao waliokaa Taanaki na miji yake, wala hao waliokaa Dori na miji yake, wala hao waliokaa Ibleamu na miji yake, wala hao waliokaa Megido na miji yake; lakini hao Wakanaani walikuwa hawakukubali kuiacha nchi hiyo.

28Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepata nguvu, ndipo walipowatia hao Wakanaani katika kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa.

29Efraimu naye hakuwatoa Wakanaani waliokuwa wakikaa katika Gezeri; lakini Wakanaani walikaa ndani ya Gezeri kati yao.

30Zabuloni naye hakuwatoa wenyeji wa Kitroni, wala hao waliokaa katika Nahalali; lakini Wakanaani walikaa kati yao, wakalazimishwa shokoa.

31Asheri naye hakuwatoa wenyeji wa Aka, wala hao waliokaa Sidoni, wala hao wa Alabu, wala hao wa Akzibu, wala hao wa Helba, wala hao wa Afeka, wala hao wa Rehobu;

32lakini Waasheri wakakaa kati ya Wakanaani, hao wenyeji wa nchi; kwa kuwa hawakuwafukuza.

33Naftali naye hakuwatoa wenyeji wa Bethshemeshi, wala hao waliokaa Bethanathi; lakini alikaa kati ya Wakanaani, hao wenyeji wa nchi; pamoja na haya hao wenyeji wa Bethshemeshi, na wenyeji wa Bethanathi, wakawatumikia kazi ya shokoa.

34Kisha Waamori waliwasukumiza wana wa Dani waende milimani; kwani hawakuwakubali kutelemkia bondeni;

35lakini hao Waamori waliendelea kukaa katika kilima cha Heresi, na katika Aiyaloni, na katika Shaalbimu; pamoja na haya mkono wa hiyo nyumba ya Yusufu ulishinda, hata wakawalazimisha shokoa.

36Mpaka wa Waamori ulikuwa tangu huko kupandia Akrabimu, tangu hilo jabali, na juu yake.