Waamuzi - Sura ya 10

Waamuzi - Sura ya 10

1Baada yake Abimeleki, akainuka Tola mwana wa Pua, mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, kuwaokoa Israeli; naye alikuwa akikaa Shamiri, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu.

2Huyo akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na mitatu, akafa, akazikwa katika Shamiri.

3Baada yake huyo akainuka Yairi, Mgileadi; naye akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na miwili.

4Huyo alikuwa na wana thelathini waliokuwa wakipanda wana-punda thelathini, nao walikuwa na miji thelathini, ambayo inaitwa Hawoth-yairi hata hivi leo, nayo iko katika nchi ya Gileadi.

5Yairi akafa, akazikwa huko Kamoni.

6Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha Bwana, wala hawakumtumikia yeye.

7Hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, akawauza na kuwaua mikononi mwa Wafilisti, na mikononi mwa wana wa Amoni.

8Nao wakawasumbua na kuwaonea wana wa Israeli mwaka huo; waliwaonea wana wa Israeli wote waliokuwa ng'ambo ya pili ya Yordani katika nchi ya Waamori, iliyoko huko Gileadi, muda wa miaka kumi na minane.

9Wana wa Amoni nao wakavuka Yordani ili wapigane na Yuda, na kupigana na Benyamini, na nyumba ya Efraimu; basi hivyo Israeli walikuwa wanasumbuliwa sana.

10Ndipo wana wa Israeli wakamlilia Bwana, wakisema, Sisi tumekufanyia dhambi, kwa sababu tumemwacha Mungu wetu, na kuyatumikia Mabaali.

11Naye Bwana akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti?

12Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao.

13Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena.

14Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu.

15Wana wa Israeli wakamwambia Bwana Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu.

16Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia Bwana; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli.

17Wakati huo wana wa Amoni walikutana pamoja, wakapanga marago huko Gileadi. Wana wa Israeli nao wakajikusanya wakapanga marago Mispa.

18Na hao watu, wakuu wa Gileadi, wakaambiana wao kwa wao, Je! Ni mtu yupi atakayeanza kupigana na wana wa Amoni? Yeye atakuwa ni kichwa juu ya wenyeji wote wa Gileadi.