Waamuzi - Sura ya 2
1Kisha malaika wa Bwana alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi;
2nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?
3Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.
4Ikawa, hapo huyo malaika wa Bwana alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia.
5Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia Bwana sadaka huko.
6Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi.
7Watu hao wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya Bwana yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
8Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi.
9Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.
10Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
11Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali.
12Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika.
13Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi.
14Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao.
15Kila walikokwenda mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika sana.
16Kisha Bwana akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara.
17Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo.
18Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.
19Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi.
20Basi hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu;
21mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa;
22ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya Bwana kwenda katika njia hiyo, au sivyo.
23Basi Bwana akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)