Waamuzi - Sura ya 8

Waamuzi - Sura ya 8

1Basi watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini wewe kututendea sisi kama haya? Hata usituite, hapo ulipokwenda kupigana na Midiani? Nao wakateta naye sana.

2Lakini akawaambia, Je! Mimi nimefanya nini sasa kama mlivyofanya ninyi? Hayo masazo ya zabibu za Efraimu si mema kuliko mavuno ya Abiezeri?

3Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi? Ndipo hasira zao walizokuwa nazo juu yake zikatulia aliposema maneno hayo.

4Basi Gideoni akafika Yordani, akauvuka, yeye na hao watu mia tatu waliokuwa pamoja naye, walikuwa wamepungukiwa na nguvu, lakini wawafuatia vivyo.

5Naye akawaambia watu wa Sukothi, Tafadhali wapeni mikate hao watu waniandamao; kwa maana wanapungukiwa na nguvu, nami ni katika kuwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.

6Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna i mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate?

7Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo Bwana atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura nyama ya miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma.

8Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu.

9Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitauvunja mnara huu.

10Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama kumi na tano elfu hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka watu mia na ishirini elfu waliokuwa wenye kutumia upanga.

11Basi Gideoni alikwea kwa njia ya hao waliokuwa wenye kukaa hemani upande wa mashariki wa Noba na Yogbeha, akalipiga hilo jeshi; kwa maana lile jeshi lilikuwa salama.

12Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanya-tapanya hilo jeshi lote.

13Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi.

14Ndipo akamshika mtu mmoja hirimu katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba.

15Kisha akawafikilia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate?

16Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo.

17Kisha akaupomosha mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo.

18Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme.

19Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mamaangu mimi; kama yeye Bwana alivyo hai, kwamba mliwaokoa hai watu hao, mimi nisingewaua ninyi.

20Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akacha, kwa sababu alikuwa ni kijana tu.

21Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao.

22Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani.

23Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye Bwana atatawala juu yenu.

24Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.)

25Wakajibu, Tutakupa kwa mioyo. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu pete za masikio ya mateka yake.

26Na uzani wa hizo pete za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia zao.

27Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake.

28Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni.

29Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe.

30Gideoni alikuwa na wana sabini waliozawa na mwili wake; kwa maana alikuwa na wake wengi.

31Na suria yake aliyekuwako Shekemu, yeye naye akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki.

32Basi Gideoni mwana wa Yoashi akafa mwenye umri wa uzee mwema, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake, katika Ofra ya Waabiezeri.

33Kisha ikawa, mara alipokufa Gideoni, wana wa Israeli wakakengeuka tena, wakawaandama Mabaali kwa ukahaba, wakamfanya Baal-berithi kuwa ni mungu wao.

34Kwani wana wa Israeli hawakumkumbuka Bwana, Mungu wao, ambaye ndiye aliyewaokoa na mikono ya adui zao wote pande zote;

35wala hawakuifanyia mema nyumba ya Yerubaali, yaani Gideoni, kwa kuyafuata hayo mema yote aliyowafanyia Israeli.