Maombolezo - Sura ya 1

Maombolezo - Sura ya 1

1Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa, Huo uliokuwa umejaa watu! Jinsi alivyokuwa kama mjane, Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa! Binti mfalme kati ya majimbo, Jinsi alivyoshikwa shokoa!

2Hulia sana wakati wa usiku, Na machozi yake yapo mashavuni; Miongoni mwa wote waliompenda Hakuna hata mmoja amfarijiye; Rafiki zake wote wamemtenda hila, Wamekuwa adui zake.

3Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa, Na kwa sababu ya utumwa mkuu; Anakaa kati ya makafiri, Haoni raha iwayo yote; Wote waliomfuata wamempata Katika dhiki yake.

4Njia za Sayuni zaomboleza, Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu; Malango yake yote yamekuwa ukiwa, Makuhani wake hupiga kite; Wanawali wake wanahuzunika; Na yeye mwenyewe huona uchungu.

5Watesi wake wamekuwa kichwa, Adui zake hufanikiwa; Kwa kuwa Bwana amemtesa Kwa sababu ya wingi wa makosa yake; Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka Mbele yake huyo mtesi.

6Naye huyo binti Sayuni Enzi yake yote imemwacha; Wakuu wake wamekuwa kama ayala Wasioona malisho; Nao wamekwenda zao hawana nguvu Mbele yake anayewafuatia.

7Siku za mateso na misiba yake, Yerusalemu huyakumbuka matamaniko yake yote Yaliyokuwa tangu siku za kale; Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi, Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia; Hao watesi wake walimwona, Wakafanya sabato zake kuwa mzaha.

8Yerusalemu amefanya dhambi sana; Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu; Wote waliomheshimu wanamdharau, Kwa sababu wameuona uchi wake; Naam, yeye anaugua, Na kujigeuza aende nyuma.

9Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake; Hakukumbuka mwisho wake; Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu; Yeye hana mtu wa kumfariji; Tazama, Bwana, teso langu; Maana huyo adui amejitukuza.

10Huyo mtesi amenyosha mkono wake Juu ya matamaniko yake yote; Maana ameona ya kuwa makafiri wameingia Ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru Wasiingie katika kusanyiko lako.

11Watu wake wote hupiga kite, Wanatafuta chakula; Wameyatoa matamaniko yao wapate chakula Cha kuihuisha nafsi; Ee Bwana, tazama, uangalie; Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.

12Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia, Angalieni, mtazame Kama kuna majonzi yo yote mfano wa majonzi yangu, Niliyotendwa mimi, Ambayo Bwana amenihuzunisha kwa hayo Siku ya hasira yake iwakayo.

13Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu, Nao umeishinda; Ametandika wavu aninase miguu, Amenirudisha nyuma; Amenifanya kuwa mtu wa pekee, Na mgonjwa mchana kutwa.

14Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake; Hayo yameshikamana; Yamepanda juu shingoni mwangu; Amezikomesha nguvu zangu;

15Bwana amenitia mikononi mwao, Ambao siwezi kupingamana nao. Bwana amewafanya mashujaa wangu wote Kuwa si kitu kati yangu; Ameita mkutano mkuu kinyume changu Ili kuwaponda vijana wangu; Bwana amemkanyaga kama shinikizoni Huyo bikira binti Yuda.

16Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji; Kwa kuwa mfariji yu mbali nami, Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa peke yao, Kwa sababu huyo adui ameshinda.

17Sayuni huinyosha mikono yake; Hakuna hata mmoja wa kumfariji; Bwana ametoa amri juu ya Yakobo, Kwamba wamzungukao wawe watesi wake; Yerusalemu amekuwa kati yao Kama kitu kichafu.

18Bwana ndiye mwenye haki; Maana nimeiasi amri yake; Sikieni, nawasihi, enyi watu wote, Mkayatazame majonzi yangu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wamechukuliwa mateka.

19Naliwaita hao walionipenda Lakini walinidanganya; Makuhani wangu na wazee wangu Walifariki mjini; Hapo walipokuwa wakitafuta chakula ili kuzihuisha nafsi zao.

20Angalia, Ee Bwana; maana mimi ni katika dhiki; Mtima wangu umetaabika; Moyo wangu umegeuka ndani yangu; Maana nimeasi vibaya sana; Huko nje upanga hufisha watu; Nyumbani mna kama mauti.

21Wamesikia kwamba napiga kite; Hakuna hata mmoja wa kunifariji; Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata; Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo; Utaileta siku ile uliyoitangaza, Nao watakuwa kama mimi.

22Huo uovu wao wote Na uje mbele zako wewe; Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi Kwa dhambi zangu zote; Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana, Na moyo wangu umezimia.