Maombolezo - Sura ya 4

Maombolezo - Sura ya 4

1Jinsi dhahabu ilivyoacha kung'aa, Na dhahabu iliyo safi ilivyobadilika! Mawe ya patakatifu yametupwa Mwanzo wa kila njia.

2Wana wa Sayuni wenye thamani, Walinganao na dhahabu safi, Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo, Kazi ya mikono ya mfinyanzi!

3Hata mbwa-mwitu hutoa matiti, Huwanyonyesha watoto wao; Binti ya watu wangu amekuwa mkali, Mfano wa mbuni jangwani.

4Ulimi wa mtoto anyonyaye Wagandamana na kaakaa lake kwa kiu; Watoto wachanga waomba chakula, Wala hakuna hata mmoja awamegeaye.

5Wale waliokula vitu vya anasa Wameachwa peke yao njiani; Wale waliokuzwa kuvaa nguo nyekundu Wakumbatia jaa.

6Maana uovu wa binti ya watu wangu ni mkubwa Kuliko dhambi ya Sodoma, Uliopinduliwa kama katika dakika moja, Wala mikono haikuwekwa juu yake.

7Wakuu wake walikuwa safi kuliko theluji, Walikuwa weupe kuliko maziwa; Miili yao, walikuwa wekundu kuliko marijani, Na umbo lao kama yakuti samawi.

8Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa; Hawajulikani katika njia kuu; Ngozi yao yagandamana na mifupa yao Imekauka, imekuwa kama mti.

9Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba.

10Mikono ya wanawake wenye huruma Imewatokosa watoto wao wenyewe; Walikuwa ndio chakula chao Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.

11Bwana ameitimiza kani yake, Ameimimina hasira yake kali; Naye amewasha moto katika Sayuni Ulioiteketeza misingi yake.

12Wafalme wa dunia hawakusadiki, Wala wote wakaao duniani, Ya kwamba mtesi na adui wangeingia Katika malango ya Yerusalemu.

13Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake Na maovu ya makuhani wake, Walioimwaga damu ya wenye haki Katikati yake.

14Hutanga-tanga njiani kama vipofu, Wametiwa unajisi kwa damu; Hata ikawa watu wasiweze Kuyagusa mavazi yao.

15Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu, Ondokeni, ondokeni, msiguse; Walipokimbia na kutanga-tanga, watu walisema kati ya mataifa, Hawatakaa hapa tena.

16Hasira ya Bwana imewatenga, Yeye hatawaangalia tena; Hawakujali nafsi za wale makuhani, Hawakuwaheshimu wazee wao.

17Macho yetu yamechoka Kwa kuutazamia bure msaada wetu; Katika kungoja kwetu tumengojea taifa Lisiloweza kutuokoa.

18Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika.

19Waliotufuatia ni wepesi Kuliko tai za mbinguni; Hao walitufuatia milimani, Nao walituotea jangwani.

20Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi

21Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu, Ukaaye katika nchi ya Usi; Hata kwako kikombe kitapita, Utalewa, na kujifanya uchi.

22Uovu wako umetimia, Ee binti Sayuni; Hatakuhamisha tena; Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu; Atazivumbua dhambi zako.