Mambo ya Walawi - Sura ya 1

Mambo ya Walawi - Sura ya 1

1Bwana akamwita Musa, na kusema naye kutoka katika hema ya kukutania, akamwambia,

2Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea Bwana matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa mifugo, katika ng'ombe na katika kondoo.

3Matoleo yake kwamba ni sadaka ya kuteketezwa ya ng'ombe, atatoa ng'ombe mume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya Bwana.

4Kisha ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya kuteketezwa; nayo itakubaliwa kwa ajili yake, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake.

5Naye atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Bwana; kisha wana wa Haruni, hao makuhani, wataileta karibu hiyo damu, na kuinyunyiza damu yake kando-kando katika madhabahu iliyo hapo mlangoni pa hema ya kukutania

6Kisha atachuna sadaka ya kuteketeza na kuikata vipande vyake.

7Kisha wana wa Haruni, watatia moto juu ya madhabahu, na kuzipanga kuni juu ya moto,

8kisha wana wa Haruni, makuhani, watazipanga kuni zilizo juu ya moto uliopo juu ya madhabahu;

9lakini matumbo yake, na miguu yake, ataiosha kwa maji; na huyo kuhani ataviteketeza vyote juu ya madhabahu, ili iwe sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.

10Na matoleo yake kwamba ni katika kundi, katika kondoo, au katika mbuzi, kuwa sadaka ya kuteketezwa; atatoa mume mkamilifu.

11Naye atamchinja hapo upande wa madhabahu ulioelekea kaskazini mbele za Bwana; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake juu ya madhabahu pande zote.

12Kisha atamkata vipande vyake, pamoja na kichwa chake, na mafuta yake; kisha atavipanga vile vipande juu ya kuni zilizo juu ya madhabahu;

13lakini matumbo yake, na miguu yake, ataosha kwa maji; na huyo kuhani atavisongeza vyote na kuviteketeza juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.

14Na matoleo yake atakayomtolea Bwana kuwa sadaka ya kuteketezwa, kwamba ni katika ndege, ndipo atakapoleta matoleo yake katika hua au katika makinda ya njiwa.

15Kisha kuhani atamleta karibu na madhabahu, naye atamkongonyoa kichwa, na kumteketeza kwa moto juu ya madhabahu; na damu yake itachuruzishwa kando ya madhabahu;

16kisha atakiondoa kile kibofu chake, pamoja na taka zake, na kukitupa kando ya madhabahu upande wa mashariki, mahali pa majivu;

17kisha atampasua na mabawa yake, lakini asimkate vipande viwili; kisha kuhani atamteketeza juu ya madhabahu, juu ya kuni zilizo juu ya moto; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.