Mambo ya Walawi - Sura ya 12

Mambo ya Walawi - Sura ya 12

1Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

2Nena na hao wana wa Israeli, uwaambie, Mwanamke akitunga mimba na kuzaa mtoto mume, ndipo atakuwa yu najisi siku saba; kama katika siku za kutengwa kwake kwa ajili ya hedhi, ndivyo atakavyokuwa najisi.

3Siku nane mtoto atatahiriwa govi ya zunga lake.

4Na huyo mwanamke atakaa katika damu ya kutakata kwake siku thelathini na tatu; asiguse kitu kilicho kitakatifu, wala asiingie mahali patakatifu, hata siku hizo za kutakata kwake zitakapotimia.

5Lakini kwamba amezaa mtoto mke ndipo atakuwa najisi juma mbili, kama katika kutengwa kwake; naye atakaa katika damu ya kutakata kwake muda wa siku sitini na sita.

6Kisha hizo siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, kwa ajili ya mwana, au kwa ajili ya binti, ataleta mwana-kondoo wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa, au hua, kuwa sadaka ya dhambi, awalete mlangoni pa hema ya kukutania, na kumpa kuhani;

7na yeye atawasongeza mbele za Bwana, na kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atatakasika na jicho la damu yake. Hii ndiyo amri yake huyo azaaye, kwamba ni mtoto mume au mke.

8Kama mali yake huyo mwanamke haimfikilii mwana-kondoo, hapo ndipo atakapochukua hua wawili, au makinda mawili ya njiwa; mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa, na wa pili kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.