Mambo ya Walawi - Sura ya 15

Mambo ya Walawi - Sura ya 15

1Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2Haya, semeni na wana wa Israeli, mkawaambie, Mtu ye yote atakapokuwa na kisonono kimtokacho mwilini mwake, atakuwa najisi kwa ajili ya kisonono chake.

3Na unajisi wake katika kisonono chake ni huu; kama mwili wake unachuruzika kisonono chake, au kama kisonono chake kimezuiwa mwilini mwake, ni unajisi wake.

4Kitanda cho chote akilaliacho mwenye kisonono kitakuwa najisi; na kitu cho chote ambacho akiketia kitakuwa najisi.

5Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo, atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

6Na mtu atakayeketi katika kitu cho chote alichokiketia mwenye kisonono, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

7Na mtu atakayegusa mwili wake mwenye kisonono atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

8Tena kama mwenye kisonono akimtemea mate mtu aliye safi; ndipo atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa yu najisi hata jioni.

9Na tandiko lo lote atakalolipanda mwenye kisonono litakuwa najisi.

10Mtu awaye yote atakayegusa kitu cho chote kilichokuwa chini yake huyo atakuwa najisi hata jioni; na mtu atakayevichukua vitu vile atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

11Na mtu ye yote atakayeguswa na mwenye kisonono, asipokuwa amenawa mikono yake majini, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

12Na chombo cha udongo ambacho amekigusa mwenye kisonono, kitavunjwa-vunjwa; na kila chombo cha mti kitaoshwa majini.

13Na huyo aliye na kisonono atakapotakaswa na kisonono chake, atajihesabia siku saba kwa kutakaswa kwake, naye atazifua nguo zake; naye ataoga mwili wake katika maji ya mtoni, naye atakuwa safi.

14Na siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, naye atakwenda mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania, naye atampa kuhani hao ndege;

15na kuhani atawasongeza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya kisonono chake.

16Na mtu ye yote akitokwa na shahawa yake, ndipo ataoga mwili wake wote majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

17Na kila nguo, na kila ngozi, ambayo ina shahawa, itafuliwa kwa maji, nayo itakuwa najisi hata jioni.

18Huyo mwanamke naye ambaye mtu mume amelala naye kwa shahawa, wote wawili wataoga majini, nao watakuwa najisi hata jioni.

19Mwanamke ye yote, kama anatokwa na kitu, na kitu chake alichokuwa nacho mwilini mwake ni damu, ataketi katika kutengwa kwake muda wa siku saba; na mtu ye yote atakayemgusa atakuwa najisi hata jioni.

20Na kitu cho chote akilaliacho katika kutengwa kwake kitakuwa najisi; na kila kitu ambacho akiketia kitakuwa najisi.

21Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo mwanamke atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

22Mtu ye yote atakayekigusa cho chote ambacho huyo mwanamke amekiketia atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

23Kwamba ni katika kitanda, au cho chote alichokikalia huyo mwanamke, atakapokigusa kitu hicho, atakuwa najisi hata jioni.

24Na mtu ye yote atakayelala na mwanamke na unajisi ukawa juu yake, atakuwa najisi muda wa siku saba; na kila kitanda alichokilalia kitakuwa najisi.

25Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo si katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatoka damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutoka damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa katika siku za kutengwa kwake; yeye yu najisi.

26Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake.

27Na mtu ye yote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

28Lakini huyo mwanamke kwamba ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi.

29Siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania.

30Kuhani atamsongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, kwa ajili ya kutoka damu ya unajisi kwake.

31Ni hivi mtakavyowatenga wana wa Israeli na unajisi wao; ili wasife katika unajisi wao, hapo watakapoitia unajisi maskani yangu iliyo katikati yao.

32Hii ndiyo sheria ya mwenye kisonono, na ya mtu ambaye shahawa yake yamtoka, akawa na unajisi kwa hiyo;

33na ya mwanamke ambaye yu katika kutengwa kwake, na ya mtu ambaye ana kisonono, kama ni mtu mume, kama ni mtu mke, na ya huyo alalaye na mwanamke mwenye unajisi.