Mambo ya Walawi - Sura ya 16

Mambo ya Walawi - Sura ya 16

1Bwana akasema na Musa, baada ya kufa kwa hao wana wawili wa Haruni, walipokaribia mbele za Bwana, wakafa;

2Bwana akamwambia Musa, Sema na Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wo wote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema.

3Haruni ataingia katika patakatifu na vitu hivi; ng'ombe mume mchanga kwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.

4Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa.

5Kisha atatwaa mikononi mwa mkutano wa Waisraeli mbuzi waume wawili, kwa sadaka ya dhambi; na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.

6Na Haruni atamtoa yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake.

7Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania.

8Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya Bwana; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli.

9Na Haruni atamleta yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Bwana, na kumtoa awe sadaka ya dhambi.

10Bali yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atawekwa hai mbele za Bwana ili kumfanyia upatanisho, ili kumpeleka jangwani kwa ajili ya Azazeli.

11Na Haruni atamsongeza ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake; naye atamchinja yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake.

12Kisha atatwaa chetezo kilichojaa makaa ya moto yatokayo katika madhabahu iliyo mbele za Bwana, na konzi mbili za uvumba mzuri uliopondwa sana, mikononi mwake, naye atauleta ndani ya pazia.

13Kisha atatia ule uvumba juu ya moto mbele za Bwana, ili moshi wa ule uvumba ukisitiri kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, asije akafa.

14Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba.

15Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema,

16naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao.

17Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli.

18Kisha atatoka na kuiendea madhabahu iliyo mbele za Bwana na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na ya damu ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote.

19Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.

20Naye akiisha kufanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, na hema ya kukutania, na madhabahu, atamleta yule mbuzi aliye hai.

21Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.

22Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani.

23Na Haruni ataingia katika hema ya kukutania, naye atavua mavazi yake ya kitani, aliyoyavaa alipoingia katika patakatifu, atayaacha humo;

24naye ataosha mwili wake kwa maji mahali patakatifu, na kuvaa nguo zake, na kutoka, na kusongeza sadaka ya kuteketezwa yake mwenyewe, na sadaka ya kuteketezwa ya watu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu.

25Na mafuta ya sadaka ya dhambi atayateketeza juu ya madhabahu.

26Na mtu yule amwachaye mbuzi wa Azazeli aende zake, ataosha nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia katika marago.

27Na yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, na yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, ambao damu yao ililetwa ndani ifanye ukumbusho katika patakatifu, watachukuliwa nje ya marago; nao watachoma moto ngozi zao, na nyama yao, na mavi yao.

28Na yeye awachomaye moto atafua nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia maragoni.

29Amri hii itakuwa amri ya milele kwenu; katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, mtajitaabisha roho zenu, msifanye kazi ya namna yo yote, mzalia na mgeni akaaye kati yenu.

30Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanywa kwa ajili yenu, ili kuwatakasa; nanyi mtatakaswa na dhambi zenu zote mbele za Bwana.

31Ni Sabato ya raha ya makini kwenu nanyi mtajitaabisha roho zenu; ni amri ya milele.

32Na kuhani atakayetiwa mafuta na kuwekwa wakfu badala ya baba yake, ataufanya huo upatanisho, naye atayavaa mavazi ya kitani, yaani, yale mavazi matakatifu.

33Naye atafanya upatanisho kwa ajili ya patakatifu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya hema ya kukutania, na kwa ajili ya madhabahu; naye atafanya upatanisho kwa ajili ya makuhani, na kwa ajili ya watu wote wa kusanyiko.

34Na amri hii itakuwa amri ya milele kwenu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao zote, mara moja kila mwaka. Naye akafanya vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa.