Mambo ya Walawi - Sura ya 20

1Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2Tena uwaambie wana wa Israeli, Mtu awaye yote miongoni mwa wana wa Israeli, au miongoni mwa wageni waketio katika Israeli, atakayetoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, sharti atauawa; wenyeji wa nchi watampiga kwa mawe.
3Mimi nami nitamkazia uso wangu mtu huyo, nami nitamkatilia mbali na watu wake; kwa kuwa ametoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, ili kupatia unajisi patakatifu pangu, na kulinajisi jina langu takatifu.
4Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu huyo kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki, wasimwue;
5ndipo mimi nitamkazia uso wangu mtu huyo, na jamaa zake, nami nitamkatilia mbali, na hao wote wamwandamao katika uzinifu, ili kufanya uzinifu pamoja na Moleki, watengwe mbali na watu wao.
6Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.
7Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
8Nanyi zishikeni sheria zangu, na kuzitenda; Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.
9Kwa maana kila mtu amlaaniye baba yake au mama yake hakika atauawa, amemlaani baba yake na mama yake; damu yake itakuwa juu yake.
10Na mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa.
11Na mtu mume atakayelala pamoja na mke wa baba yake amefunua utupu wa baba yake; wote wawili hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao.
12Na mtu mume akilala na mkwewe mwanamke wote wawili hakika watauawa; wamefanya yaliyo uchafuko; damu yao itakuwa juu yao.
13Tena mtu mume akilala pamoja na mtu mume, kama alalavyo na mtu mke, wote wawili wamefanya machukizo; hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao.
14Tena mtu mume akimwoa mke pamoja na mama yake, ni uovu mkuu; watachomwa moto, yeye mume na hao wanawake pia; ili kwamba usiwe uovu kati yenu.
15Tena mtu mume akilala na mnyama, hakika atauawa; nanyi mtamwua huyo mnyama.
16Tena mwanamke akimkaribia mnyama ye yote, na kulala pamoja naye, mtamwua huyo mwanamke, na mnyama pia; hakika watauawa; damu yao itakuwa ni juu yao.
17Tena mtu mume akimwoa umbu lake, binti ya baba yake, au binti ya mama yake, na kuuona utupu wake, na huyo mwanamke kauona utupu wake huyo mume; ni jambo la aibu; watakatiliwa mbali mbele ya macho ya wana wa watu wao; amefunua utupu wa umbu lake; naye atauchukua uovu wake.
18Tena mtu mume akilala na mwanamke aliye na ugonjwa wake, na kufunua utupu wake; amelifunua jito la damu yake, naye mwanamke amefunua jito la damu yake; wote wawili watakatiliwa mbali na watu wao.
19Usifunue utupu wa umbu la mama yako, wala umbu la baba yako; kwa kuwa huyo amefunua utupu wa jamaa yake ya karibu; watauchukua uovu wao.
20Tena mtu mume akilala na mke wa mjomba wake, ameufunua utupu wa mjomba wake; watauchukua uovu wao; watakufa bila kuzaa mwana.
21Tena mtu mume akimtwaa mke wa nduguye, ni uchafu; ameufunua utupu wa nduguye; hao watakuwa hawana wana.
22Basi zishikeni amri zangu zote, na hukumu zangu zote, na kuzifanya; ili kwamba hiyo nchi, ambayo nawapeleka ninyi kukaa, isiwatapike.
23Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.
24Lakini mimi nimewaambia ninyi, Mtairithi nchi yao, nami nitawapa ninyi kuimiliki; nchi iliyojaa maziwa na asali; mimi ni Bwana, Mungu wenu, niliyewatenga ninyi na mataifa.
25Kwa ajili ya hayo mtapambanua kati ya mnyama aliye safi na mnyama aliye najisi, na kati ya ndege aliye tohara na ndege aliye najisi; nanyi msizifanye nafsi zenu kuwa machukizo kwa njia ya mnyama, au kwa njia ya ndege, au kwa njia ya kitu cho chote ambacho nchi imejaa nacho, niliowatenga nanyi kuwa ni najisi.
26Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.
27Tena mtu mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe; damu yao itakuwa juu yao.