Mambo ya Walawi - Sura ya 21

Mambo ya Walawi - Sura ya 21

1Kisha Bwana akamwambia Musa, Nena na hao makuhani, wana wa Haruni, uwaambie, Mtu asijinajisi kwa ajili ya wafu katika watu wake;

2isipokuwa ni kwa ajili ya jamaa yake wa karibu, kwa ajili ya mama yake, na kwa ajili baba yake, na kwa ajili ya mwanawe, na kwa ajili ya binti yake, na kwa ajili ya nduguye mwanamume;

3na kwa ajili ya umbu lake aliye mwanamwali, aliye wa udugu kwake, ambaye hajaolewa na mume; ana ruhusa kujitia unajisi kwa ajili yake huyo.

4Asijitie unajisi, ijapokuwa ni mkubwa katika watu wake, hata akajinajisi.

5Wasijifanyie upaa kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje chale katika miili yao.

6Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala wasilinajisi jina la Mungu wao; kwa kuwa wao ndio wasongezao sadaka za Bwana kwa njia ya moto, chakula cha Mungu wao; kwa ajili ya hayo watakuwa watakatifu.

7Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake.

8Kwa hiyo basi utamtakasa; kwa kuwa yeye husongeza chakula cha Mungu wako; atakuwa mtakatifu kwako wewe; kwa kuwa mimi Bwana niwatakasaye ninyi ni mtakatifu.

9Na binti ya kuhani ye yote atakapojitia unajisi kwa ukahaba, amemtia unajisi baba yake; atachomwa moto.

10Na yeye aliye kuhani mkuu katika nduguze, ambaye mafuta ya kutiwa yamemiminwa kichwani mwake, naye akawekwa wakfu ili ayavae hayo mavazi, yeye hataziacha wazi nywele za kichwa chake, wala hatazirarua nguo zake;

11wala hataingia penye maiti, wala asijitie unajisi kwa ajili ya baba yake wala mama yake;

12wala asitoke katika mahali patakatifu, wala asipatie unajisi mahali patakatifu pa Mungu wake; kwa kuwa utakaso wa hayo mafuta ya kutiwa ya Mungu wake u juu yake; mimi ndimi Bwana.

13Naye atamwoa mwanamke katika ubikira wake.

14Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe.

15Naye asiwatie unajisi kizazi chake katika watu wake; kwa kuwa mimi ndimi Bwana nimtakasaye.

16Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

17Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.

18Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili,

19au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono,

20au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;

21mtu awaye yote wa kizazi cha Haruni kuhani aliye na kilema asikaribie kuzisongeza sadaka za Bwana kwa njia ya moto; ana kilema huyo asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.

22Atakula chakula cha Mungu wake, katika hicho kilicho kitakatifu sana, na hicho kilicho kitakatifu.

23Lakini hataingia ndani ya pazia, wala asikaribie madhabahu, kwa sababu ana kilema; ili kwamba asipanajisi patakatifu pangu; kwa kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye.

24Basi Musa akanena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote.