Mambo ya Walawi - Sura ya 6

1Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya Bwana, akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la kunyang'anya, au kumwonea mwenziwe;
3au kuzumbua kitu kilichopotea na kutenda la uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo;
4ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang'anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokizumbua yeye,
5au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia.
6Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa Bwana, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani;
7na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.
8Bwana akanena na Musa na kumwambia,
9Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike.
10Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu.
11Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi.
12Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.
13Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.
14Na amri ya hiyo sadaka ya unga ni hii; wana wa Haruni wataisongeza mbele za Bwana, mbele ya madhabahu.
15Naye atatwaa konzi yake katika huo unga, katika huo unga mwembamba wa sadaka ya unga, na katika mafuta yake, na ubani wote ulio juu ya sadaka ya unga, kisha atauteketeza juu ya madhabahu kuwa harufu ya kupendeza, kuwa ukumbusho wake kwa Bwana.
16Na unga uliosalia Haruni na wanawe wataula; utaliwa pasipo kutiwa chachu, katika mahali patakatifu; katika ua wa hema ya kukutania ndipo watakapoula.
17Hautaokwa na chachu. Nimewapa kuwa sehemu yao katika matoleo yangu yasongezwayo kwa njia ya moto; ni kitu kitakatifu sana, kama hiyo sadaka ya dhambi, na kama hiyo sadaka ya hatia.
18Kila mwana mume miongoni mwa wana wa Haruni atakula katika huo, kuwa ni haki yao milele katika vizazi vyenu, katika matoleo ya Bwana yasongezwayo kwa njia ya moto; mtu awaye yote atakayevigusa atakuwa ni mtakatifu
19Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
20Matoleo ya Haruni na wanawe watakayomtolea Bwana, katika siku atakayotiwa mafuta, ni haya; sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga daima, nusu yake asubuhi, na nusu yake jioni.
21Utaandaliwa kaangoni pamoja na mafuta; ukisha kulowama utauleta ndani; utasongeza hiyo sadaka ya unga vipande vilivyookwa, iwe harufu ya kupendeza kwa Bwana.
22Na huyo kuhani aliyetiwa mafuta badala yake katika hao wanawe ataisongeza; itateketezwa kabisa kwa Bwana kwa amri ya milele.
23Tena kila sadaka ya unga ya kuhani itateketezwa kabisa; isiliwe.
24Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
25Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya hiyo sadaka ya dhambi ni hii; mahali hapo pachinjwapo sadaka ya kuteketezwa ndipo itakapochinjwa sadaka ya dhambi, mbele za Bwana; ni takatifu sana.
26Huyo kuhani atakayeisongeza kwa ajili ya dhambi ndiye atakayeila; italiwa katika mahali patakatifu, katika ua wa hema ya kukutania.
27Kila kitu kitakachoigusa nyama ya sadaka hiyo kitakuwa kitakatifu; tena itakapomwagika damu yake yo yote katika nguo yo yote, utaifua nguo hiyo iliyomwagiwa, katika mahali patakatifu.
28Lakini hicho chombo cha udongo ambacho hiyo nyama ilipikwa ndani yake kitavunjwa; na kama ikipikwa katika chombo cha shaba, kitasuguliwa, na kuoshwa kwa maji.
29Kila mwana mume miongoni mwa makuhani atakula katika hiyo; ni takatifu sana.
30Wala haitaliwa sadaka ya dhambi yo yote, ambayo damu yake yo yote ililetwa ndani ya hema ya kukutania, ili kufanya upatanisho katika mahali patakatifu; itachomwa moto.