Mambo ya Walawi - Sura ya 8

Mambo ya Walawi - Sura ya 8

1Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

2Mtwae Haruni, na wanawe pamoja naye, na yale mavazi, na mafuta ya kutia, na ng'ombe mume wa sadaka ya dhambi, na kondoo waume wawili, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu;

3kisha ukutanishe mkutano wote hapo mlangoni pa hema ya kukutania.

4Basi Musa akafanya kama alivyoambiwa na Bwana; na huo mkutano ulikutanishwa mlangoni pa hema ya kukutania.

5Musa akawaambia mkutano, Neno aliloliagiza Bwana kwamba lifanywe, ni hili.

6Basi Musa akawaleta Haruni na wanawe, akawaosha kwa maji.

7Kisha akamvika Haruni ile kanzu, na kumfunga mshipi, na kumvika joho, na kumvika naivera, na kumfunga huo mshipi wa kazi ya mstadi wa naivera na kumfunga naivera kwa huo mshipi.

8Kisha akamtia kile kifuko cha kifuani; akatia hizo Urimu na Thumimu katika hicho kifuko cha kifuani.

9Akamvika na kile kilemba kichwani mwake; na juu ya kilemba, upande wa mbele, akakitia kile kipande cha dhahabu, hiyo taji takatifu; kama Bwana alivyomwagiza Musa.

10Kisha Musa akatwaa hayo mafuta matakatifu ya kutia, akatia mafuta maskani, na vyote vilivyokuwamo, na kuvitakasa.

11Kisha akanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kuitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake, ili kuvitakasa.

12Kisha akamimina mafuta hayo ya kutia kichwani mwake Haruni, na kumtia mafuta, ili amtakase.

13Kisha Musa akawaleta wana wa Haruni, na kuwavika kanzu, na kuwafunga mishipi, na kuwavika vilemba; kama Bwana alivyomwagiza Musa.

14Kisha akamleta yule ng'ombe mume wa sadaka ya dhambi; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao katika kichwa cha huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi.

15Kisha akamchinja; na Musa akaitwaa damu yake, akaitia katika pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake, akaitakasa madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu, na kuitakasa, ili afanye upatanisho kwa ajili yake.

16Kisha akayatwaa mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo yake, na kitambi kilichokuwa katika ini, na figo zake mbili, na mafuta yake, na Musa akayateketeza juu ya madhabahu.

17Lakini huyo ng'ombe mwenyewe, na ngozi yake, na nyama yake, na mavi yake, akayachoma moto nje ya marago; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.

18Kisha akamsongeza yule kondoo mume wa sadaka ya kuteketezwa; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.

19Kisha akamchinja; na Musa akainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.

20Kisha akamkata kondoo vipande vyake; na Musa akateketeza kichwa, na vile vipande, na mafuta.

21Kisha akayaosha matumbo na miguu yake kwa maji; na Musa akamteketeza huyo kondoo wote juu ya madhabahu; ilikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza; ilikuwa ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto; kama Bwana alivyomwagiza Musa.

22Kisha akamsongeza kondoo mume wa pili, huyo kondoo wa kuwaweka wakfu; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.

23Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume.

24Kisha akawaleta wana wa Haruni, na Musa akaitia hiyo damu katika ncha za masikio ya kuume, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vya gumba vya maguu yao ya kuume; kisha Musa akainyunyiza hiyo damu katika madhabahu pande zote.

25Kisha akayatwaa hayo mafuta, na mkia wenye mafuta, na mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo, na kitambi cha ini, na figo mbili, na mafuta yake, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume;

26kisha katika kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichokuwa pale mbele za Bwana, akatwaa mkate mmoja usiochachwa, na mkate mmoja ulioandaliwa na mafuta na kaki moja nyembamba, akaiweka juu ya mafuta, na juu ya huo mguu wa nyuma wa upande wa kuume;

27kisha akaweka vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe, na kuvitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana.

28Kisha Musa akavitwaa tena mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa vilikuwa vya kuwaweka wakfu, ni harufu nzuri; ilikuwa dhabihu iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto.

29Kisha Musa akakitwaa kile kidari, akakitikisa huku na huku, kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; ni sehemu ya Musa katika huyo kondoo mume wa kuwaweka wakfu; kama Bwana alivyomwagiza Musa.

30Kisha Musa akatwaa baadhi ya mafuta ya kutia, na ya damu iliyokuwa pale juu ya madhabahu, na kumnyunyizia Haruni, katika mavazi yake, na wanawe, katika mavazi yao, pamoja naye; akamtakasa Haruni, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.

31Kisha Musa akawaambia huyo Haruni na wanawe, Tokoseni hiyo nyama mlangoni pa hema ya kukutania; mkaile pale pale, na hiyo mikate iliyo katika kile kikapu cha kuwaweka wakfu, kama nilivyoagizwa kusema, Haruni na wanawe wataila.

32Nacho kitakachosalia katika hiyo nyama na mikate mtakichoma moto.

33Wala msitoke nje mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba, hata siku za kuwekwa wakfu kwenu zitakapotimia; kwa kuwa atawaweka muda wa siku saba.

34Vile vile kama vilivyotendeka siku ya leo, ni vivyo Bwana alivyoagiza kufanywa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.

35Nanyi mtakaa mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba mchana na usiku, na kuulinda ulinzi wa Bwana ili kwamba msife; kwani ndivyo nilivyoagizwa.

36Basi Haruni na wanawe wakafanya mambo hayo yote Bwana aliyoyaagiza kwa mkono wa Musa.