Luka - Sura ya 1

Luka - Sura ya 1

1Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu,

2kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,

3nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu,

4upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.

5Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.

6Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.

7Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.

8Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,

9kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.

10Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba.

11Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.

12Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.

13Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.

14Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.

15Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.

16Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.

17Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.

18Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi.

19Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.

20Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.

21Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni.

22Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu.

23Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake.

24Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema,

25Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.

26Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti,

27kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.

28Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.

29Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?

30Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.

31Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.

32Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.

33Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.

34Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?

35Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.

36Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa;

37kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.

38Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

39Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,

40akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.

41Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu;

42akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.

43Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?

44Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.

45Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.

46Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

47Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;

48Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;

49Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu.

50Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha.

51Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

52Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza.

53Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.

54Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake;

55Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele.

56Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

57Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume.

58Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye.

59Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria.

60Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana.

61Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo.

62Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita.

63Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote.

64Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu.

65Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi.

66Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

67Na Zakaria, baba yake, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema,

68Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa.

69Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.

70Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;

71Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;

72Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu;

73Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,

74Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,

75Kwa utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote.

76Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake;

77Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao.

78Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia,

79Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.

80Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.