Luka - Sura ya 11

Luka - Sura ya 11

1Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.

2Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.]

3Utupe siku kwa siku riziki yetu.

4Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu].

5Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,

6kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;

7na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?

8Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.

9Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.

10Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.

11Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?

12Au akimwomba yai, atampa nge?

13Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

14Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu.

15Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.

16Wengine walimjaribu, wakimtaka ishara itokayo mbinguni.

17Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka.

18Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli.

19Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu.

20Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.

21Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama;

22lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.

23Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya.

24Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema,

25Nitairudia nyumba yangu niliyotoka.

26Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.

27Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya.

28Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.

29Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona.

30Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki.

31Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka ncha za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani.

32Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.

33Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga.

34Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza.

35Angalia basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.

36Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga wake.

37Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani.

38Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula.

39Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu.

40Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia?

41Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.

42Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.

43Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni.

44Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo.

45Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi.

46Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.

47Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua.

48Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara.

49Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza,

50ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu;

51tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki.

52Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.

53Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi,

54wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.