Luka - Sura ya 12

Luka - Sura ya 12

1Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki.

2Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana.

3Basi, yo yote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari.

4Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi.

5Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo.

6Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu.

7Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

8Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu;

9na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.

10Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema;

12kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema.

13Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.

14Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?

15Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.

16Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;

17akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.

18Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.

19Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.

20Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?

21Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

22Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini.

23Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi.

24Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege!

25Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?

26Basi, ikiwa hamwezi hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine?

27Yatafakarini maua jinsi yameavyo; hayatendi kazi wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.

28Basi, ikiwa Mungu huvika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatawatendea ninyi zaidi, enyi wa imani haba?

29Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi,

30kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo.

31Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa.

32Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.

33Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.

34Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu.

35Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;

36nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.

37Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia.

38Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.

39Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa.

40Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.

41Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?

42Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake?

43Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo.

44Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote.

45Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa;

46bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.

47Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.

49Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?

50Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!

51Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano.

52Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu.

53Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.

54Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

55Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.

56Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?

57Na mbona ninyi wenyewe kwa nafsi zenu hamwamui yaliyo haki?

58Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani.

59Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.