Luka - Sura ya 13

Luka - Sura ya 13

1Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.

2Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?

3Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.

4Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?

5Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.

6Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.

7Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?

8Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi;

9nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.

10Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo.

11Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.

12Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.

13Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.

14Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato.

15Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha?

16Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?

17Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.

18Kisha alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini?

19Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.

20Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu?

21Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.

22Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu.

23Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia,

24Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;

26ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.

27Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

28Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje.

29Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.

30Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.

31Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua.

32Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.

33Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.

34Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka.

35Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.