Luka - Sura ya 18

Luka - Sura ya 18

1Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

2Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.

4Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

6Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.

7Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

8Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?

9Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.

10Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.

11Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

12Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.

13Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.

14Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

15Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea.

16Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao.

17Amin, nawaambia, Mtu ye yote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe.

18Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele?

19Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu.

20Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako.

21Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu.

22Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate.

23Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi.

24Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!

25Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

26Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?

27Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.

28Petro akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata.

29Akawaambia, Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu,

30asiyepokea zaidi mara nyingi katika zamani hizi, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

31Akawachukua wale Thenashara, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote yatatimizwa, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii.

32Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate;

33nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka.

34Walakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa.

35Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka;

36na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini?

37Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita.

38Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.

39Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu.

40Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza,

41Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona.

42Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.

43Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.