Luka - Sura ya 23

Luka - Sura ya 23

1Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato.

2Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.

3Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema.

4Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.

5Nao walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku.

6Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya.

7Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile.

8Na Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye.

9Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote.

10Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana.

11Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato.

12Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao.

13Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu,

14akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki;

15wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilolitenda lipasalo kufa.

16Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [

17Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.]

18Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba.

19Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji

20Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu.

21Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe.

22Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.

23Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda.

24Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike.

25Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.

26Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.

27Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.

28Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.

29Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha.

30Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni.

31Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

32Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.

33Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto.

34Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.

35Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake.

36Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,

37huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.

38Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

39Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

40Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?

41Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.

42Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.

43Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.

44Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,

45jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.

46Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

47Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.

48Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua.

49Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.

50Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki;

51(wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu;

52mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu.

53Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake.

54Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia.

55Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa.

56Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.