Luka - Sura ya 3

Luka - Sura ya 3

1Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene,

2wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria, jangwani.

3Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi,

4kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya; Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.

5Kila bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa;

6Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.

7Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?

8Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto.

9Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

10Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi?

11Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo.

12Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi?

13Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa.

14Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.

15Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo,

16Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto;

17ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.

18Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu.

19Lakini mfalme Herode alipokaripiwa na yeye kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, na maovu yote aliyoyafanya Herode,

20aliongeza na hili juu ya yote, alimfunga Yohana gerezani.

21Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka;

22Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

23Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli,

24wa Mathati, wa Lawi, wa Melki, wa Yana, wa Yusufu,

25wa Matathia, wa Amosi, wa Nahumu, wa Esli, wa Nagai,

26wa Maathi, wa Matathia, wa Semei, wa Yusufu, wa Yuda,

27wa Yoana, wa Resa, wa Zerubabeli, wa Shealtieli, wa Neri,

28wa Melki, wa Adi, wa Kosamu, wa Elmadamu, wa Eri,

29wa Yoshua, wa Eliezeri, wa Yorimu, wa Mathati, wa Lawi,

30wa Simeoni, wa Yuda, wa Yusufu, wa Yonamu, wa Eliakimu,

31wa Melea, wa Mena, wa Matatha, wa Nathani, wa Daudi,

32wa Yese, wa Obedi, wa Boazi, wa Salmoni, wa Nashoni,

33wa Aminadabu, wa Aramu, wa Hesroni, wa Peresi, wa Yuda,

34wa Yakobo, wa Isaka, wa Ibrahimu, wa Tera, wa Nahori,

35wa Serugi, wa Ragau, wa Pelegi, wa Eberi, wa Sala,

36wa Kenani, wa Arfaksadi, wa Shemu, wa Nuhu, wa Lameki,

37wa Methusela, wa Henoko, wa Yaredi, wa Mahalaleli, wa Kenani,

38wa Enoshi, wa Sethi, wa Adamu, wa Mungu.