Malaki - Sura ya 2

Malaki - Sura ya 2

1Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi.

2Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema Bwana wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni.

3Angalieni, nitaikemea mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam, mavi ya sadaka zenu; nanyi mtaondolewa pamoja nayo

4Nanyi mtajua ya kuwa mimi nimewapelekeeni amri hii, ili agano langu liwe na Lawi, asema Bwana wa majeshi.

5Agano langu naye lilikuwa agano la uhai na amani; nami nikampa ili aogope, naye akaniogopa, akalicha jina langu.

6Sheria ya kweli ilikuwa kinywani mwake, wala udhalimu haukuonekana midomoni mwake; alikwenda pamoja nami katika amani na unyofu, na kuwageuza wengi hata wakaacha uovu.

7Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake; kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bwana wa majeshi.

8Bali ninyi mmegeuka mkaiacha njia; mmewakwaza watu wengi katika sheria; mmeliharibu agano la Lawi, asema Bwana wa majeshi.

9Kwa sababu hiyo mimi nami nimewafanya ninyi kuwa kitu cha kudharauliwa, na unyonge, mbele ya watu wote, kama vile ninyi msivyozishika njia zangu, bali mmewapendelea watu katika sheria.

10Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu?

11Yuda ametenda kwa hiana, na chukizo limetendeka katika Israeli, na katika Yerusalemu; maana Yuda ameunajisi utakatifu wa Bwana aupendao, naye amemwoa binti ya mungu mgeni.

12Bwana atamtenga mtu atendaye hayo, yeye aliye macho, na yeye ajibuye, atamtenga na hema za Yakobo, pia atamtenga yeye amtoleaye Bwana wa majeshi dhabihu.

13Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya Bwana kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia.

14Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako.

15Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana.

16Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.

17Mmemchokesha Bwana kwa maneno yenu. Lakini ninyi mwasema, Tumemchokesha kwa maneno gani? Kwa kuwa mwasema, Kila atendaye mabaya ni mwema machoni pa Bwana, naye huwafurahia watu hao, au, Mungu mwenye kuhukumu yuko wapi?