Malaki - Sura ya 4

1Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.
2Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini.
3Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu; katika siku ile niifanyayo, asema Bwana wa majeshi.
4Ikumbukeni torati ya Musa, mtumishi wangu, niliyomwamuru huko Horebu kwa ajili ya Israeli wote, naam, amri na hukumu.
5Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya.
6Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.