Marko - Sura ya 11

Marko - Sura ya 11

1Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake,

2akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni.

3Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa.

4Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua.

5Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda?

6Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.

7Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake.

8Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani.

9Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;

10umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.

11Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara.

12Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa.

13Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.

14Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.

15Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa;

16wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu.

17Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.

18Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake.

19Na kulipokuwa jioni alitoka mjini.

20Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani.

21Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka.

22Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu.

23Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.

24Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.

25Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.

26Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]

27Wakafika Yerusalemu tena; hata alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee,

28wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?

29Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.

30Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni.

31Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini?

32Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, -- waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi.

33Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.