Marko - Sura ya 15

1Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato.
2Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema.
3Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi.
4Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki!
5Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.
6Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye.
7Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile.
8Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea.
9Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi?
10Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda.
11Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba.
12Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi?
13Wakapiga kelele tena, Msulibishe.
14Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe.
15Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe.
16Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima.
17Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani;
18wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!
19Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia.
20Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe.
21Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.
22Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa.
23Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee.
24Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini.
25Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha.
26Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI.
27Na pamoja naye walisulibisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [
28Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.]
29Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu,
30jiponye nafsi yako, ushuke msalabani.
31Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe.
32Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea.
33Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa.
34Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
35Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya.
36Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha.
37Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.
38Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini.
39Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
40Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome;
41hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.
42Hata ikiisha kuwa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato,
43akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu.
44Lakini Pilato akastaajabu, kwamba amekwisha kufa. Akamwita yule akida, akamwuliza kwamba amekufa kitambo.
45Hata alipokwisha kupata hakika kwa yule akida, alimpa Yusufu yule maiti.
46Naye akanunua sanda ya kitani, akamtelemsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi.
47Nao Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose wakapatazama mahali alipowekwa.