Marko - Sura ya 3

Marko - Sura ya 3

1Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza;

2wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki.

3Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati.

4Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza.

5Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena.

6Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza.

7Naye Yesu akajitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi,

8na Yerusalemu, na Idumaya, na ng'ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea.

9Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga.

10Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa.

11Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.

12Akawakataza sana, wasimdhihirishe.

13Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea.

14Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri,

15tena wawe na amri ya kutoa pepo.

16Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro;

17na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo;

18na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo,

19na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti. Kisha akaingia nyumbani.

20Mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate.

21Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.

22Nao waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo.

23Akawaita, akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani?

24Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama;

25na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama.

26Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo.

27Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake.

28Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote;

29bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,

30kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu.

31Wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita.

32Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka, wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.

33Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani?

34Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu!

35Kwa maana mtu ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.