Marko - Sura ya 7

Marko - Sura ya 7

1Kisha Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake,

2wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa.

3Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao;

4tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba.

5Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?

6Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami;

7Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu,

8Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.

9Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu.

10Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe.

11Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi;

12wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye;

13huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.

14Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu.

15Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu.

16Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.]

17Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano.

18Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi;

19kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote.

20Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.

21Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati,

22wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.

23Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.

24Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika.

25Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake.

26Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake.

27Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa.

28Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.

29Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako.

30Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.

31Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli.

32Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono.

33Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi,

34akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka.

35Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri.

36Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari;

37wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.