Marko - Sura ya 8

Marko - Sura ya 8

1Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia,

2Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula;

3nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali.

4Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?

5Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba,

6Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano.

7Walikuwa na visamaki vichache; akavibarikia, akasema wawaandikie na hivyo pia.

8Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba.

9Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga.

10Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.

11Wakatokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu.

12Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki.

13Akawaacha, akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng'ambo.

14Wakasahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu.

15Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.

16Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate.

17Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito?

18Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki?

19Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili.

20Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba.

21Akawaambia, Hamjafahamu bado?

22Wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse.

23Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu?

24Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda.

25Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi.

26Akampeleka nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie.

27Akatoka Yesu na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani?

28Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii.

29Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo.

30Akawaonya wasimwambie mtu habari zake.

31Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.

32Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea.

33Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.

34Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.

35Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.

36Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

37Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?

38Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.