Matayo - Sura ya 12

Matayo - Sura ya 12

1Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala.

2Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato.

3Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe?

4jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao?

5Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia?

6Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.

7Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia.

8Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.

9Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao.

10Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Wapate kumshitaki.

11Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa?

12Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato.

13Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaunyosha, ukapona, ukawa mzima kama wa pili.

14Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza.

15Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote,

16akawakataza wasimdhihirishe;

17ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,

18Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu.

19Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani.

20Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda.

21Na jina lake Mataifa watalitumainia.

22Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona.

23Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi?

24Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.

25Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama.

26Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?

27Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu.

28Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.

29Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake.

30Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.

31Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.

32Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.

33Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana.

34Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake.

35Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya.

36Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.

37Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.

38Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.

39Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.

40Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.

41Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona.

42Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.

43Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.

44Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.

45Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.

46Alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje, wataka kusema naye.

47Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe.

48Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani?

49Akawanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu!

50Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.