Matayo - Sura ya 15

Matayo - Sura ya 15

1Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema,

2Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula.

3Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?

4Kwa kuwa Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe.

5Bali ninyi husema, Atakayemwambia babaye au mamaye, Cho chote kikupasacho kusaidiwa na mimi ni wakfu,

6basi asimheshimu baba yake au mama yake. Mkalitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu.

7Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema,

8Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.

9Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.

10Akawaita makutano akawaambia

11Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi.

12Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa?

13Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.

14Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.

15Basi Petro akajibu, akamwambia, Tueleze mfano huo.

16Yesu akasema, Hata sasa ninyi nanyi mngali hamna akili?

17Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?

18Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano;

20hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi.

21Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.

22Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.

23Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.

24Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

25Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.

26Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.

27Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.

28Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

29Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko.

30Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya;

31hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli.

32Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani.

33Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii?

34Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache.

35Akawaagiza mkutano waketi chini;

36akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano.

37Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa.

38Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila wanawake na watoto.

39Akawaaga makutano, akapanda chomboni, akaenda pande za Magadani.