Matayo - Sura ya 22

Matayo - Sura ya 22

1Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema,

2Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.

3Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja.

4Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.

5Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;

6nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.

7Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.

8Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.

9Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.

10Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.

11Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.

12Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa.

13Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

14Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

15Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.

16Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.

17Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?

18Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?

19Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari.

20Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?

21Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.

22Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.

23Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza,

24wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao.

25Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake.

26Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba.

27Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.

28Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye.

29Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.

30Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni.

31Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema,

32Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai.

33Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake.

34Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja.

35Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu;

36Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?

37Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

38Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

39Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

40Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.

41Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo?

42Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi.

43Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema,

44Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako?

45Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe?

46Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena.