Matayo - Sura ya 5

Matayo - Sura ya 5

1Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia;

2akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,

3Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

4Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika.

5Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.

6Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.

7Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.

8Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.

9Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.

10Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

11Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.

12Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

13Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.

14Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.

15Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.

16Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

17Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.

18Kwa maana, amin,

19Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

20Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

21Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.

22Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.

23Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,

24iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.

25Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.

26Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.

27Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;

28lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

29Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.

30Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.

31Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka;

32lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.

33Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;

34lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;

35wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.

36Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

37Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.

38Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;

39Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.

40Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.

41Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.

42Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.

43Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

44lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

45ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.