Mika - Sura ya 1

Mika - Sura ya 1

1Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Mika, Mmorashti, katika siku za Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; maono aliyoyaona katika habari za Samaria, na Yerusalemu.

2Sikilizeni, enyi watu wa kabila zote; sikiliza, Ee dunia, na vyote vilivyomo; Bwana MUNGU na ashuhudie juu yenu, yeye Bwana kutoka hekalu lake takatifu.

3Kwa maana, angalieni, Bwana anakuja akitoka mahali pake, naye atashuka, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka.

4Na hiyo milima itayeyuka chini yake, nayo mabonde yatapasuliwa, kama vile nta iliyo mbele ya moto, kama maji yaliyomwagika tena kutelemka gengeni.

5Kwa sababu ya kosa la Yakobo yametokea haya yote, na kwa sababu ya makosa ya nyumba ya Israeli. Nini kosa la Yakobo? Je, silo Samaria? Na nini mahali pa Yuda palipoinuka? Sipo Yerusalemu?

6Kwa ajili ya hayo nitafanya Samaria kuwa kama chungu katika shamba, na kama miche ya shamba la mizabibu; nami nitayatupa mawe yake bondeni, nami nitaifunua misingi yake.

7Na sanamu zake zote za kuchonga zitapondwa-pondwa, na ijara zake zote zitateketezwa kwa moto, na sanamu zake zote nitazifanya ukiwa; kwa kuwa amezikusanya kwa ujira wa kahaba, nazo zitaurudia ujira wa kahaba.

8Kwa ajili ya hayo nitaomboleza na kulia, Nitakwenda nimevua nguo, ni uchi; Nitafanya mlio kama wa mbweha, Na maombolezo kama ya mbuni.

9Kwa maana jeraha zake haziponyekani; Maana msiba umeijilia hata Yuda, Unalifikia lango la watu wangu, Naam, hata Yerusalemu.

10Msiyahubiri haya katika Gathi, msilie kamwe; Katika Beth-le-Afra ugae-gae mavumbini.

11Piteni; uende ukaaye Shafiri, hali ya uchi na aibu; Hivyo akaaye Saanani hajatokea nje; Maombolezo ya Beth-eseli yatawaondolea tegemeo lake;

12Maana akaaye Marothi ana utungu wa mema; Kwa kuwa msiba umeshuka toka kwa Bwana, Umefika mpaka lango la Yerusalemu.

13Mfungie gari la vita farasi Aliye mwepesi, ukaaye Lakishi; Alikuwa mwanzo wa dhambi kwa binti Sayuni; Maana makosa ya Israeli yameonekana kwako.

14Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi zawadi ya kuagia; Nyumba za Akzibu zitakuwa kijito kidanganyacho wafalme wa Israeli.

15Bado, ukaaye Maresha, nitakuletea yeye atakayekumiliki; Utukufu wa Israeli utafika mpaka Adulamu.

16Jifanyie upaa, jikate nywele zako, Kwa ajili ya watoto waliokufurahisha; Panua upaa wako kama tai; Kwa maana wamekwenda mbali nawe utumwani.