Mika - Sura ya 5

Mika - Sura ya 5

1Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye amemhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo.

2Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.

3Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli.

4Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.

5Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtaondokesha wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.

6Nao wataiharibu nchi ya Ashuru kwa upanga, na nchi ya Nimrodi katika malango yake; naye atatuokoa na Mwashuri, atakapoingia katika nchi yetu, na kukanyaga ndani ya mipaka yetu.

7Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya kabila nyingi mfano wa umande utokao kwa Bwana, mfano wa manyunyu katika manyasi; yasiyomngojea mtu, wala kuwakawilia wanadamu.

8Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya mataifa, kati ya kabila nyingi, mfano wa simba kati ya wanyama wa msituni, kama mwana-simba kati ya makundi ya kondoo, ambaye, akiwa anapita katikati, hukanyaga-kanyaga na kurarua-rarua, wala hakuna wa kuokoa.

9Mkono wako na uinuliwe juu ya adui zako, na adui zako wote wakauliwe mbali.

10Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema Bwana, nitawakatilia mbali farasi zako watoke kati yako, nami nitayaharibu magari yako ya vita;

11nami nitaikatilia mbali miji ya nchi yako, na ngome zako zote nitaziangusha;

12nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana;

13nami nitakatilia mbali sanamu zako na nguzo zako, zitoke kati yako; wala hutaiabudu tena kazi ya mikono yako.

14Nami nitayang'oa maashera yenu, yasiwe kati yako; nami nitaiangamiza miji yako.

15Nami nitajilipiza kisasi katika hasira na ghadhabu juu ya mataifa wasiosikiliza.