Nehemia - Sura ya 11

Nehemia - Sura ya 11

1Basi, wakuu wa watu walikuwa wakikaa Yerusalemu; nao watu waliosalia wakapiga kura, ili katika watu kumi kumleta mmoja akae ndani ya Yerusalemu mji mtakatifu, na wale kenda wakae mijini.

2Na hao watu wakawabariki wote waliojitoa kwa hiari wakae Yerusalemu.

3Basi hawa ndio wakuu wa jimbo waliokaa Yerusalemu; ila mijini mwa Yuda wakakaa kila mtu katika milki yake mijini mwao, yaani, Israeli, makuhani, na Walawi, na Wanethini, na akina watumwa wa Sulemani.

4Tena wakakaa Yerusalemu wengine wa wana wa Yuda, na wengine wa wana wa Benyamini. Wa wana wa Yuda; Athaya, mwana wa Uzia, mwana wa Zekaria, mwana wa Amaria, mwana wa Shefatia, mwana wa Mahalaleli, wa wana wa Peresi;

5na Maaseya, mwana wa Baruki, mwana wa Kolhoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zekaria, Mshelani.

6Wana wa Peresi wote waliokaa Yerusalemu walikuwa watu mia nne sitini na wanane, mashujaa.

7Na wana wa Benyamini ndio hawa; Salu, mwana wa Meshulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Maaseva, mwana wa Ithieli, mwana wa Yeshaya.

8Na baada yake Gabai, Salai,

9Na Yoeli, mwana wa Zikri, alikuwa msimamizi wao; na Yuda, mwana wa Hasenua, alikuwa wa pili juu ya mji.

10Wa makuhani; Yedaya, Yoyaribu, Yakini,

11na Seraya, mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu, msimamizi wa nyumba ya Mungu,

12na ndugu zao waliofanya kazi ya nyumbani, watu mia nane ishirini na wawili; na Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amzi, mwana wa Zekaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya,

13na ndugu zake, wakuu wa mbari za mababa, watu mia mbili arobaini na wawili; na Maasai, mwana wa Azareli, mwana wa Azai, mwana wa Meshilemothi, mwana wa Imeri,

14na ndugu zao, waume mashujaa, watu mia na ishirini na wanane; na msimamizi wao alikuwa Zabdieli, mmojawapo wa hao wakuu.

15Na wa Walawi; Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, mwana wa Buni;

16na Shabethai na Yozabadi, wa wakuu wa Walawi, walioisimamia kazi ya nje ya nyumba ya Mungu;

17na Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zikri, mwana wa Asafu, mkuu mwenye kuanzisha shukrani katika sala, na Bakbukia, wa pili wake miongoni mwa nduguze; na Obadia, mwana wa Shemaya, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni.

18Walawi wote waliokaa katika mji mtakatifu walikuwa watu mia mbili themanini na wanne.

19Pamoja na hao, mabawabu; Akubu, Talmoni, na ndugu zao waliolinda malangoni, walikuwa watu mia na sabini na wawili.

20Na Israeli waliosalia, katika hao makuhani, na Walawi, walikuwamo mijini mwote mwa Yuda, kila mtu katika milki yake.

21Lakini Wanethini walikuwa wakikaa Ofeli; na juu ya Wanethini walikuwa Siha na Gishpa.

22Naye msimamizi wa Walawi huko Yerusalemu, ni Uzi, mwana wa Bani, mwana wa Hashabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika, wa wana wa Asafu, hao waimbaji, alikuwa juu ya kazi ya nyumba ya Mungu.

23Kwa kuwa palikuwa na amri ya mfalme juu yao, na agizo la hakika walilowekewa waimbaji, kama ilivyohusika na kila siku.

24Na Pethahia, mwana wa Meshezabeli, wa wana wa Zera, mwana wa Yuda, alikuwa wakili wa mfalme kwa habari ya mambo yote ya watu.

25Na katika habari za vijiji na mashamba yake; wengine wa wana wa Yuda walikuwa wakikaa Kiriath-arba na vijiji vyake, na katika Diboni na vijiji vyake, na Yekabzeeli na vijiji vyake;

26na katika Yeshua, na Molada, na Beth-peleti;

27na Hazar-shuali, na Beer-sheba na vijiji vyake;

28na katika Siklagi, na Mekona na vijiji vyake;

29na katika Enrimoni, na Sora, na Yarmuthi;

30Zanoa, Adulamu na vijiji vyake, Lakishi na mashamba yake, Azeka na vijiji vyake. Hivyo wakatua toka Beer-sheba mpaka bonde la Hinomu.

31Wana wa Benyamini nao walikuwa wakikaa Geba, na Mikmashi, na Aiya, na Beth-eli na vijiji vyake;

32Anathothi, Nobu, Anania;

33Hazori, Rama, Gitaimu;

34Hadidi, Seboimu, Nebalati;

35Lodi, na Ono, bonde la Wakarashi.

36Na wa Walawi, wengine walikaa katika Yuda na wengine katika Benyamini.