Nehemia - Sura ya 13

Nehemia - Sura ya 13

1Siku hiyo walisoma katika kitabu cha Musa masikioni mwa watu; na ndani yake yalionekana maneno haya yameandikwa, ya kwamba Mwamoni na Mmoabi wasiingie katika kusanyiko la Mungu milele;

2kwa sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa baraka.

3Ikawa walipoisikia torati, wakawatenga Israeli na umati wa watu waliochanganyika nao.

4Na kabla ya hayo, Eliashibu, kuhani, aliyewekwa avisimamie vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, kwa kuwa alikuwa karibu yake Tobia,

5alikuwa amemtengenezea chumba kikubwa, hapo walipoweka zamani sadaka za unga, na ubani, na vyombo, na zaka za nafaka, na divai, na mafuta, walivyoamriwa kuwapa Walawi, na waimbaji, na mabawabu; tena sadaka za kuinuliwa zilizokuwa za makuhani.

6Lakini wakati huo wote mimi sikuwako huko Yerusalemu; maana katika mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta, mfalme wa Babeli, nalimrudia mfalme; na baada ya siku kadha wa kadha nikaomba ruhusa tena kwa mfalme.

7Nami nikaja Yerusalemu, nikafahamu yale mabaya, ambayo Eliashibu ameyatenda kwa ajili ya Tobia, kwa kumtengenezea chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.

8Nami nikasikitika sana; basi nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia vitoke humo chumbani.

9Kisha nikatoa amri, nao wakavisafisha vyumba; nami nikavirudisha humo vyombo vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za unga na ubani.

10Tena nikaona ya kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao; basi wamekimbia Walawi na waimbaji, waliofanya kazi, kila mtu shambani kwake.

11Ndipo nikagombana na mashehe, nikasema, Mbona nyumba ya Mungu imeachwa? Kisha nikawakusanya, nikawaweka mahali pao.

12Ndipo Yuda wote walipoleta zaka za nafaka, na mvinyo, na mafuta, kwenye hazina.

13Nami nikawaweka watunza hazina juu ya hazina, yaani, Shelemia kuhani, na Sadoki mwandishi, na wa Walawi, Pedaya; na wa pili wao alikuwa Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania; kwani walihesabiwa kuwa waaminifu, na ilikuwa juu yao kuwagawia ndugu zao.

14Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, na kwa taratibu zake.

15Siku hizo naliona katika Yuda watu wengine waliokanyaga mashinikizo ya mvinyo siku ya sabato, na wengine waliochukua miganda, na kuwapakia punda zao; tena na mvinyo, na zabibu, na tini, na namna zote za mizigo, waliyoileta Yerusalemu, siku ya sabato; nami nikashuhudia juu yao siku ile waliyouza vyakula.

16Tena wakakaa humo watu wa Tiro, walioleta samaki, na biashara za kila namna, wakawauzia wana wa Yuda siku ya sabato, na mumo humo Yerusalemu.

17Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato?

18Je! Sivyo hivyo walivyofanya baba zenu; na Mungu wetu, je! Hakuyaleta mabaya haya yote juu yetu, na juu ya mji huu? Nanyi hata hivyo mwazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi sabato!

19Ikawa malango ya Yerusalemu yalipoanza kuwa na giza kabla ya sabato, naliamuru milango ifungwe, nikaamuru isifunguliwe hata sabato iishe; na baadhi ya watumishi wangu nikawaweka juu ya malango, ili usiingizwe mzigo wo wote siku ya sabato.

20Basi wenye biashara na wachuuzi wa bidhaa za kila namna wakalala nje ya Yerusalemu mara mbili tatu.

21Ndipo nikawashuhudia, nikawaambia, Mbona mwalala mbele ya ukuta? Mkitenda hivi tena, nitawakamata. Tangu wakati ule hawakuja tena siku ya sabato.

22Kisha nikawaamuru Walawi wajitakase, nao waje kuyalinda malango, ili kuitakasa siku ya sabato. Unikumbukie hayo nayo, Ee Mungu wangu, ukaniachilie sawasawa na wingi wa rehema zako.

23Tena siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na Amoni, na Moabu;

24na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo.

25Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.

26Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye.

27Basi, na sisi, je! Tuwasikilize ninyi kutenda neno hili baya, hata kumhalifu Mungu wetu kwa kuwaoa wanawake wageni?

28Na mwana mmoja wa Yoyada, mwana wa Eliashibu, kuhani mkuu, alikuwa mkwewe Sanbalati, Mhoroni, basi nikamfukuza kwangu.

29Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, jinsi walivyounajisi ukuhani, na agano la ukuhani na la Walawi.

30Hivyo nikawatakasa na kila kitu kigeni, nami nikawaagizia zamu makuhani na Walawi, kila mtu kazini mwake;

31na matoleo ya kuni nyakati zilizoamriwa, na malimbuko. Nikumbuke, Ee Mungu wangu, ili unitendee mema.