Hesabu - Sura ya 10

1Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2Jifanyie tarumbeta mbili za fedha; utazifanya za kazi ya ufuzi; nawe utazitumia kwa kuwaita mkutano wakutane, na kwa kusafiri kwao yale makambi.
3Na hapo watakapozipiga hizo tarumbeta, mkutano wote utakukutanikia wewe, hapo mlangoni pa hema ya kukutania.
4Nao wakipiga tarumbeta moja tu ndipo wakuu, walio vichwa vya maelfu ya Israeli, watakukutanikia wewe
5Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha sana, marago yaliyoko upande wa mashariki yatasafiri. Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha ya pili, marago yaliyoko upande wa kusini watasafiri;
6watapiga sauti ya kugutusha kwa ajili ya safari zao.
7Lakini mkutano utakapokutanishwa pamoja mtapiga, lakini hamtapiga sauti ya kugutusha.
8Wana wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta; nazo zitakuwa kwenu ni amri ya milele katika vizazi vyenu vyote.
9Tena hapo mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu.
10Tena katika siku ya furaha yenu, na katika sikukuu zenu zilizoamriwa, na katika kuandama miezi kwenu, mtapiga hizo tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa, na juu ya dhabihu za sadaka zenu za amani; nazo zitakuwa kwenu ni ukumbusho mbele za Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
11Ikawa mwaka wa pili, mwezi wa pili, siku ya ishirini ya mwezi, hilo wingu liliinuka kutoka pale juu ya maskani ya ushahidi.
12Wana wa Israeli wakasafiri kwenda mbele, kwa safari zao kutoka jangwa la Sinai; na hilo wingu likakaa katika jangwa la Parani.
13Nao wakasafiri kwanza kwa amri ya Bwana kwa mkono wa Musa.
14Mahali pa mbele ilisafiri beramu ya marago ya wana wa Yuda, kwa majeshi yao; na Nashoni mwana wa Aminadabu ndiye aliyekuwa juu ya jeshi lake.
15Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Isakari alikuwa Nethaneli mwana wa Suari.
16Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni.
17Na maskani ilishushwa; na wana wa Gershoni, na wana wa Merari, walioichukua maskani, wakasafiri kwenda mbele.
18Kisha beramu ya marago ya Reubeni ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri.
19Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Suri-shadai.
20Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli.
21Ndipo wakasafiri Wakohathi wenye kuvichukua vile vitu vitakatifu; na hao wengine wakaisimamisha maskani kabla hawajaja wao.
22Kisha beramu ya marago ya wana wa Efraimu ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Elishama mwana wa Amihudi.
23Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri.
24Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni.
25Kisha beramu ya marago ya wana wa Dani, ambayo yalikuwa ni nyuma ya marago yote, ikasafiri, kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Ahiezeri mwana wa Amishadai.
26Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani;
27Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani.
28Ndivyo zilivyokuwa safari zao wana wa Israeli kwa majeshi: yao; nao wakasafiri kwenda mbele.
29Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo Bwana amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa Bwana ametamka mema juu ya Israeli.
30Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe.
31Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho.
32Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote Bwana atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo.
33Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa Bwana safari ya siku tatu; na sanduku la agano la Bwana likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika.
34Na wingu la Bwana lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini.
35Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee Bwana, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao.
36Tena hapo liliposimama, akasema, Ee Bwana, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.