Hesabu - Sura ya 13

Hesabu - Sura ya 13

1Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,

2Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao.

3Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na Bwana; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli.

4Na majina yao ni haya; katika kabila ya Reubeni, Shamua mwana Zakuri.

5Katika kabila ya Simeoni, Shafati mwana wa Hori.

6Katika kabila ya Yuda, Kalebu mwana wa Yefune.

7Katika kabila ya Isakari, Igali mwana wa Yusufu.

8Katika kabila ya Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni

9Katika kabila ya Benyamini, Palti mwana wa Rafu.

10Katika kabila ya Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi.

11Katika kabila ya Yusufu, yaani, katika kabila ya Manase, Gadi mwana wa Susi.

12Katika kabila ya Dani, Amieli mwana wa Gemali.

13Katika kabila ya Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli.

14Katika kabila ya Naftali, Nabi mwana wa Wofsi.

15Katika kabila ya Gadi, Geueli mwana wa Maki.

16Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua.

17Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani,

18mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi;

19na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome;

20nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza.

21Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi.

22Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri.

23Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini.

24Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli.

25Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini.

26Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi.

27Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake.

28Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko.

29Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.

30Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.

31Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi.

32Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.

33Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.