Hesabu - Sura ya 17

Hesabu - Sura ya 17

1Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,

2Nena na wana wa Israeli, kisha upokee kwao fimbo, fimbo moja kwa ajili ya nyumba ya kila baba, katika wakuu wao wote, kama nyumba za baba zao zilivyo, fimbo kumi na mbili; kisha andika jina la kila mtu katika fimbo yake.

3Na katika fimbo ya Lawi utaliandika jina la Haruni; maana, itakuwa fimbo moja kwa kila kichwa cha nyumba za baba zao.

4Nawe utaziweka katika hema ya kukutania mbele ya huo ushahidi, hapo nikutanapo pamoja nanyi.

5Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manung'uniko ya wana wa Israeli, wanung'unikiayo juu yenu.

6Basi Musa akawaambia wana wa Israeli, ndipo wakuu wao wote wakampa fimbo, fimbo moja kwa kila mkuu, kama nyumba za baba zao zilivyokuwa, fimbo kumi na mbili; na fimbo ya Haruni ilikuwa kati ya fimbo zao.

7Kisha Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana katika hema ya kukutania.

8Ilikuwa siku ya pili yake, Musa akaingia ndani ya hema ya ushahidi; na tazama, ile fimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa malozi mabivu.

9Kisha Musa akazileta nje hizo fimbo zote kutoka hapo mbele za Bwana na kuziweka mbele ya wana wa Israeli wote; nao wakaangalia, na kila mtu akaitwaa fimbo yake.

10Kisha Bwana akamwambia Musa, Irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili itunzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung'uniko yao waliyoninung'unikia, ili wasife.

11Basi Musa akafanya vivyo; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo alivyofanya.

12Kisha wana wa Israeli wakanena na Musa, na kumwambia, Angalia, sisi twafa, twaangamia, sote twaangamia.

13Kila mtu akaribiaye, aikaribiaye maskani ya Bwana, hufa; je! Tutakufa pia sote?