Hesabu - Sura ya 18

1Bwana akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu.
2Na ndugu zako nao, kabila ya Lawi, kabila ya baba yako, uwalete karibu pamoja nawe, ili waungwe nawe, na kukuhudumia; bali wewe na wanao pamoja nawe mtakuwa mbele ya hema ya ushahidi.
3Nao watashika ulinzi kwa amri yako, na ulinzi wa Hema yote; lakini wasikaribie vyombo vya patakatifu, wala madhabahu, wasife, wao pamoja na ninyi.
4Nao wataungwa nawe, na kuushika ulinzi wa hema ya kukutania, kwa ajili ya utumishi wote wa hema; na mgeni asiwakaribie ninyi.
5Nanyi mtashika ulinzi wa patakatifu, na ulinzi wa madhabahu, isiwe ghadhabu juu ya wana wa Israeli tena.
6Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa Bwana, waufanye utumishi wa hema ya kukutania.
7Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa.
8Kisha Bwana akamwambia Haruni, Tazama, nimekupa wewe ulinzi wa sadaka zangu za kuinuliwa, maana, vitu vyote vya hao wana wa Israeli vilivyowekwa wakfu; nimekupa wewe na wanao vitu hivyo kwa ajili ya kule kutiwa mafuta kwenu, kuwa haki yenu milele.
9Vitu hivi vitakuwa vyako katika vile vilivyo vitakatifu sana, visiteketezwe motoni; matoleo yao yote, maana, kila sadaka yao ya unga, na kila sadaka yao ya dhambi, na kila sadaka yao ya hatia watakayonitolea, vitakuwa vitakatifu sana kwa ajili yako wewe na kwa wanao.
10Utakula vitu hivyo kuwa ni vitu vitakatifu sana; kila mume atakula vitu hivyo; vitakuwa vitakatifu kwako wewe.
11Tena kitu hiki ni chako; ile sadaka ya kuinuliwa ya kipawa chao, maana, sadaka za kutikiswa zote za wana wa Israeli; hizi nimekupa wewe, na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu milele; kila mtu katika nyumba yako aliye safi atakula katika hizo.
12Yaliyo mazuri katika mafuta, na yaliyo mazuri ya mavuno ya zabibu, na ya mavuno ya nafaka, malimbuko yake watakayompa Bwana, amekupa wewe hayo.
13Matunda ya kwanza yaivayo katika yote yaliyo katika nchi yao, watakayomletea Bwana, yatakuwa yako, kila mtu aliye safi katika nyumba yako atakula katika vitu hivyo.
14Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako.
15Kila kifunguacho tumbo, cha wenye mwili wote watakachomsongezea Bwana cha wanadamu na cha wanyama, ni chako; lakini mzaliwa wa kwanza wa binadamu, huna budi utamkomboa, na mzaliwa wa kwanza wa wanyama wasio safi utamkomboa.
16Na hao watakaokombolewa katika wanyama hao, tangu aliyepata umri wa mwezi mmoja utamkomboa, kama utakavyohesabu kima chake, kwa fedha ya shekeli tano, kwa shekeli ya mahali patakatifu (nayo ni gera ishirini).
17Lakini mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe, au mzaliwa wa kwanza wa kondoo, au mzaliwa wa kwanza wa mbuzi, hutawakomboa hao; maana, ni watakatifu hao; utanyunyiza damu yao katika madhabahu, na kuyateketeza mafuta yao kuwa sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto, iwe harufu ya kupendeza.
18Tena nyama yao itakuwa ni yako wewe, kama kile kidari cha kutikiswa, na kama mguu wa nyuma wa upande wa kuume, itakuwa yako.
19Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa Bwana, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za Bwana kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe.
20Kisha Bwana akamwambia Haruni, Wewe hutakuwa na urithi katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lo lote kati yao; mimi ni fungu lako, na urithi wako, katika wana wa Israeli.
21Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania.
22Mwanzo wa sasa wana wa Israeli wasikaribie hema ya kukutania, wasije wakachukua dhambi, nao wakafa.
23Lakini Walawi watatumika utumishi wa hema ya kukutania, nao watauchukua uovu wao; hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu vyote, na kati ya wana wa Israeli hawatakuwa na urithi.
24Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi uwao wote.
25Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
26Tena utanena na Walawi, na kuwaambia, Hapo mtakapoitwaa zaka mkononi mwa wana wa Israeli niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi wenu, ndipo mtakaposongeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka.
27Na sadaka yenu ya kuinuliwa itahesabiwa kwenu, kama ndiyo nafaka ya sakafu ya kupuria, na kama kujaa kwake kinu cha kushindikia zabibu.
28Hivyo ninyi nanyi mtasongeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana katika zaka zenu zote, mpokeazo mikononi mwa wana wa Israeli; kwa hiyo mtampa Haruni kuhani hiyo sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana.
29Katika vipawa vyenu vyote mtasongeza kila sadaka ya kuinuliwa ya Bwana, ya wema wake wote, hiyo sehemu yake iliyowekwa takatifu.
30Kwa ajili ya hayo utawaambia, Mtakapoinua humo hayo yaliyo mema, ndipo yatahesabiwa kuwa ya Walawi, kama kuongea kwake sakafu ya kupuria nafaka, na kama maongeo ya kinu cha kushindikia zabibu.
31Nanyi mtakula hayo kila mahali, ninyi na watu wa nyumbani mwenu; kwa kuwa ni thawabu yenu badala ya utumishi wenu katika hema ya kukutania.
32Nanyi hamtachukua dhambi kwa ajili yake, hapo mtakapokwisha kuinua humo hayo mema yake; lakini msivitie unajisi vile vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, ili msife.