Hesabu - Sura ya 20

Hesabu - Sura ya 20

1Kisha wana wa Israeli, mkutano wote, wakaingia bara ya Sini, katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadeshi; Miriamu akafa huko, akazikwa huko.

2Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni.

3Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana!

4Mbona mmewaleta kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu?

5Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa.

6Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa Bwana ukawatokea.

7Bwana akasema na Musa, akinena,

8Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao.

9Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru.

10Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu?

11Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.

12Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.

13Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na Bwana, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao.

14Kisha Musa akatuma wajumbe kutoka Kadeshi wamwendee mfalme wa Edomu, na kusema, Ndugu yako Israeli asema, Wewe wazijua taabu zote zilizotupata;

15jinsi baba zetu walivyotelemkia Misri, nasi tulikaa Misri muda mwingi, nao Wamisri walitutenda vibaya sana, na baba zetu pia;

16tena tulipomlilia Bwana, akatusikiza sauti yetu, akamtuma malaika, na kututoa tutoke Misri; nasi tupo hapa Kadeshi, mji wa mpakani mwako mwa mwisho;

17tafadhali utupe ruhusa tupite katika nchi yako; hatutapita katika mashamba, wala katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visimani; tutaifuata njia kuu ya mfalme, tusigeuke kwenda upande wa kuume, wala upande wa kushoto, hata tutakapopita mpaka wako.

18Edomu akamwambia, Hutapita katika nchi yangu, nisije nikakutokea kupigana nawe kwa upanga.

19Wana wa Israeli wakamwambia, Tutakwea kwa njia kuu; tena kama tukinywa maji yako, mimi na wanyama wangu wa mifugo, ndipo nitakulipa thamani yake; nipe ruhusa nipite kwa miguu yangu wala sitaki neno lingine lo lote.

20Akamwambia, Hutapita katika nchi yangu. Kisha Edomu akamtokea ili kupigana naye, na watu wengi, na kwa mkono wa nguvu.

21Basi hivyo Edomu akakataa kumpa Israeli ruhusa kupita katika mipaka yake; kwa hivyo Israeli akageuka na kumwacha.

22Kisha wakasafiri kutoka Kadeshi; wana wa Israeli, mkutano mzima, wakafikilia mlima wa Hori.

23Bwana akanena na Musa na Haruni katika mlima wa Hori, karibu na mpaka wa nchi ya Edomu, akawaambia,

24Haruni atakusanywa awe pamoja na watu wake; kwa kuwa hataingia katika nchi niliyowapa wana wa Israeli, kwa sababu mliasi kinyume cha neno langu hapo penye maji ya Meriba.

25Uwatwae Haruni na mwanawe Eleazari uwalete juu ya mlima wa Hori;

26umvue Haruni mavazi yake, ukamvike Eleazari mwanawe mavazi hayo; kisha Haruni atakusanywa kwa watu wake, naye atakufa huko.

27Musa akafanya kama Bwana alivyomwagiza; wakakwea katika mlima wa Hori mbele ya macho ya mkutano wote.

28Kisha Musa akamvua Haruni mavazi yake, akamvika mwanawe Eleazari mavazi hayo; Haruni akafa huko katika kilele cha mlima; Musa na Eleazari wakatelemka mlimani.

29Na mkutano wote ulipoona ya kuwa Haruni amekufa, wakamwombolea Haruni muda wa siku thelathini, maana, nyumba yote ya Israeli ikamwombolea.