Hesabu - Sura ya 23

1Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.
2Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
3Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima.
4Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
5Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya.
6Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye.
7Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli.
8Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?
9Kutoka kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa.
10Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo, Au kuhesabu robo ya Israeli? Na nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake.
11Balaki akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa kabisa.
12Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu?
13Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko.
14Akamchukua mpaka shamba la Sofimu, hata kilele cha Pisga, akajenga madhabahu saba, akatoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
15Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami nitaonana na Bwana kule.
16Bwana akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki, ukaseme hivi.
17Akafika kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu pamoja naye. Balaki akamwambia, Bwana amenena nini?
18Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori;
19Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?
20Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua.
21Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao.
22Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati.
23Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!
24Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba mke, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hata atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa.
25Balaki akamwambia Balaamu, Basi usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa.
26Lakini Balaamu akajibu akamwambia Balaki, Je! Sikukuambia ya kwamba, Kila neno Bwana atakalolisema sina budi kulitenda?
27Kisha Balaki akamwambia Balaamu, Haya, njoo sasa, nikupeleke mahali pengine; labda Mungu ataridhia kwamba unilaanie watu hao huko.
28Basi Balaki akamchukua Balaamu akaenda naye mpaka kilele cha mlima Peori, mahali paelekeapo upande wa nyika iliyo chini yake.
29Balaamu akamwambia Balaki, Haya, unijengee hapa madhabahu saba, kisha uniandalie ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.
30Basi Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, akasongeza sadaka ng'ombe mume na kondoo mume juu ya kila madhabahu.