Hesabu - Sura ya 24

Hesabu - Sura ya 24

1Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani.

2Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia.

3Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema;

4Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho;

5Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli!

6Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda Bwana, Mfano wa mierezi kando ya maji.

7Maji yatafurika katika ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa.

8Mungu amemleta kutoka Misri, Ana nguvu mfano wa nguvu za nyati; Atawameza mataifa walio adui zake, Ataivunja mifupa yao vipande vipande. Atawachoma kwa mishale yake.

9Aliinama, akalala mfano wa simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemstusha? Na abarikiwe kila akubarikiye, Na alaaniwe kila akulaaniye.

10Hasira ya Balaki ikawaka juu ya Balaamu akayapiga makofi; Balaki akamwambia Balaamu, Nalikuita ili unilaanie adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi.

11Basi sasa kimbilia mahali pako; naliazimu kukuheshimu sana; lakini, tazama, Bwana amekuzuilia heshima.

12Balaamu akamwambia Balaki, Je! Sikuwaambia wajumbe wako ulionipelekea, nikisema,

13Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, kutenda neno jema, wala neno baya, kwa nia yangu mwenyewe; Bwana atakalolinena ndilo nitakalolinena mimi.

14Basi sasa, tazama, ninakwenda kwa watu wangu; haya, nitakuarifu mambo ambayo watu hawa watakayowatenda watu wako siku za mwisho.

15Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema,

16Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho,

17Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia.

18Na Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli watakapotenda kwa ushujaa.

19Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo, Atawaangamiza watakaobaki mjini.

20Kisha akamwangalia Amaleki, akatunga mithali yake, akasema, Amaleki alikuwa ni wa kwanza wa mataifa; Lakini mwisho wake atafikilia uharibifu.

21Kisha akamwangalia Mkeni, akatunga mithali yake, akasema, Makao yako yana nguvu, Na kitundu chako kimewekwa katika jabali.

22Pamoja na haya Wakeni wataangamizwa, Hata Ashuru atakapokuchukua mateka.

23Akatunga mithali yake akasema, Ole wao! Ni nani atakayepona, Mungu atakapofanya haya?

24Lakini merikebu zitakuja kutoka pwani kwa Kitimu, Nazo zitamtaabisha Ashuru, na Eberi zitamtaabisha, Yeye naye atafikilia uharibifu.

25Basi Balaamu akainuka, akaondoka na kurudi mahali pake; Balaki naye akaenda zake.