Hesabu - Sura ya 3

Hesabu - Sura ya 3

1Basi vizazi vya Haruni na Musa, siku hiyo Bwana aliyosema na Musa katika mlima wa Sinai, ni hivi.

2Tena majina ya hao wana wa Haruni ni haya; Nadabu mzaliwa wa kwanza, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.

3Hayo ndiyo majina ya wana wa Haruni, hao makuhani waliotiwa mafuta, ambao aliwaweka wakfu ili wafanye kazi ya ukuhani.

4Kisha Nadabu na Abihu walikufa mbele za Bwana, waliposongeza moto wa kigeni mbele za Bwana, katika bara ya Sinai, nao walikuwa hawana wana; na Eleazari na Ithamari wakafanya kazi ya ukuhani mbele ya uso wa Haruni baba yao.

5Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

6Ilete karibu kabila ya Lawi, ukawaweke mbele ya Haruni kuhani, ili wapate kumtumikia.

7Nao wataulinda ulinzi wake, na ulinzi wa mkutano wote mbele ya hema ya kukutania, ili watumike utumishi wa maskani.

8Nao watavitunza vyombo vyote vya hema ya kukutania, na kulinda ulinzi wa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa maskani.

9Nawe utawapa Haruni na wanawe hao Walawi wawe nao; amepewa watu hao kabisa kwa ajili ya wana wa Israeli.

10Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa.

11Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

12Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu;

13kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi Bwana.

14Kisha Bwana akanena na Musa huko katika bara ya Sinai, na kumwambia,

15Uwahesabu wana wa Lawi kwa kuandama nyumba za baba zao na jamaa zao; kila mtu mume tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi utawahesabu.

16Basi Musa akawahesabu kama neno la Bwana kama alivyoagizwa.

17Na wana wa Lawi walikuwa ni hawa kwa majina yao; Gershoni, na Kohathi, na Merari.

18Na majina ya wana wa Gershoni kwa jamaa zao ni Libni na Shimei.

19Na wana wa Kohathi kwa jamaa zao ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli.

20Na wana wa Merari kwa jamaa zao ni Mahli, na Mushi. Hizi ndizo jamaa za Walawi kwa nyumba za baba zao.

21Katika Gershoni walikuwa jamaa ya Walibni, na jamaa ya Washimei, hawa ndio jamaa za Wagershoni.

22Hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, hao waliohesabiwa kwao walikuwa saba elfu na mia tano.

23Jamaa za Wagershoni watapanga rago nyuma ya maskani, upande wa magharibi.

24Na mkuu wa nyumba ya baba zao Wagershoni atakuwa Eliasafu mwana wa Laeli.

25Na ulinzi wa Wagershoni katika hema ya kukutania ni hiyo maskani, na Hema, na kifuniko chake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania,

26na kuta za nguo za ua, na sitara ya mlango wa ua, iliyo karibu na maskani, na karibu na madhabahu pande zote, na kamba zake zitumiwazo kwa matumizi yake yote.

27Na katika Kohathi ni jamaa ya Waamrami, na jamaa ya Waishari, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya hao Wauzieli; hizo ni jamaa za Wakohathi.

28Kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa elfu nane na mia sita, wenye kuulinda ulinzi wa mahali patakatifu.

29Jamaa za wana wa Kohathi watapanga rago upande wa kusini wa maskani.

30Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Wakohathi atakuwa Elisafani mwana wa Uzieli.

31Na vitu watakavyovitunza ni hilo sanduku, na meza, na kinara cha taa, na madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu wavitumiavyo katika kutumika kwao, na pazia, na utumishi wake wote.

32Na Eleazari mwana wa Haruni kuhani atakuwa mkuu wa hao wakuu wa Walawi, naye atawasimamia hao walindao ulinzi wa mahali patakatifu.

33Katika Merari ni jamaa ya hao Wamahli, na jamaa ya Wamushi; hizo ni jamaa za Merari.

34Na hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa sita elfu na mia mbili.

35Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Merari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hao watapanga rago upande wa maskani, wa kaskazini.

36Na usimamizi walioamriwa wana wa Merari ulikuwa ni kutunza mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake, na vyombo vyake vyote, na utumishi wake wote;

37na nguzo za ua zilizouzunguka, na matako yake, na vigingi vyake, na kamba zake.

38Na hao watakaopanga mbele ya maskani upande wa mashariki, mbele ya hema ya kukutania upande wa kuelekea maawio ya jua, watakuwa hawa, Musa na Haruni na wanawe, wenye kulinda ulinzi wa mahali patakatifu, yaani, huo ulinzi wa wana wa Israeli; na mgeni atakayekaribia atauawa.

39Hao wote waliohesabiwa katika Walawi, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana, kwa jamaa zao, waume wote tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa ishirini na mbili elfu.

40Kisha Bwana akamwambia Musa, Uwahesabu waume wote wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi uyahesabu majina yao.

41Nawe utawatwaa Walawi kwa ajili yangu mimi (Mimi ndimi Bwana) badala ya hao wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli; na wanyama wa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama wa wana wa Israeli.

42Musa akahesabu, kama Bwana alivyomwagiza, wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli.

43Wazaliwa wa kwanza wote walio waume kwa hesabu ya majina, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, katika hao waliohesabiwa kwao, walikuwa ishirini na mbili elfu na mia mbili na sabini na watatu.

44Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

45Uwatwae Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli, na wanyama wa Walawi badala ya wanyama wao; na hao Walawi watakuwa wangu mimi; mimi ndimi Bwana.

46Tena kwa kuwakomboa hao watu mia mbili na sabini na watatu, wa hao wazaliwa wa kwanza wa Israeli, ambao wamezidi ile hesabu ya Walawi,

47utatwaa shekeli tano kwa kichwa cha kila mtu kwa hiyo shekeli ya mahali patakatifu (shekeli ni gera ishirini);

48na hizo fedha ambazo waliosalia wamekombolewa kwazo utampa Haruni na wanawe.

49Basi Musa akawatoza fedha za ukombozi, hao waliozidi hesabu ya wale waliokombolewa na Walawi;

50akatwaa hizo fedha kwa wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli; shekeli elfu moja na mia tatu na sitini na tano kwa shekeli ya mahali patakatifu;

51kisha hizo fedha za ukombozi Musa akampa Haruni na wanawe, kama neno la Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Musa.